(+video) Mchungaji amlazimisha mwanaume kuanguka chini wakati wa maombi

Mchungaji huyo alionekana kumsuka mwanaume huyo ili aanguke, alipogoma kuanguka mchungaji akampiga mweleka na kumpeleka chini.

Muhtasari

• Mwanaume huyo alionekana kugoma kabisa kutekeleza takwa la mchungaji ambapo mtumishi wa Mungu alilazimika kumshika kwa fujo na kumpeleka chini.

Mchungaji mmoja amezua tafrani mitandaoni baada ya video yake akimlazimisha jamaa mmoja muumini ili kuanguka chini wakati wa maombi ya toba.

Katika klipu hiyo iliyozua mjadala mkali haswa kwenye mtandao wa Twitter, mchungaji huyo ambaye ni mfupi kidogo kwa kimo kuliko mwanaume huyo alionekana akimgusa gusa huyo muumini kama njia moja na kumshawishi kujiangusha chini.

Mwanaume huyo alionekana kugoma kabisa kutekeleza takwa la mchungaji ambapo mtumishi wa Mungu alilazimika kumshika kwa fujo na kumpiga mweleka mmoja matata uliomsafirisha sakafuni.

Kama hilo halitoshi, mchungaji huyo alimkalia muumini kifuani kama maigizo kwenye michezo ya masumbwi kabla ya kumuinua tena na kumbeba hobela hobela mabegani. Alikimbia naye na kumtua kwenye safu ya viti kwa kishindo utadhani ni hamali akibwaga gunia la mpunga uliokauka.

Wakati hayo yakiendelea, waumini wengine walikuwa wanaendelea na kuimba nyimbo za kuabudu huku wengine wakionekana macho yao kutokwa pima katika kile mchungaji na muumini walikuwa wanafanya kama maigizo ya filamu.

Video hiyo iliyopakiwa kwenye mtandao wa Twitter ilivutia maoni kinzani kutoka kwa watu, baadhi wakihisi mwanaume huyo alifeli kujiangusha ili kumdhihirishia mchungaji uwezo wake wa kufanya miujiza kwa kuwafanya watu wapukutike chini kama majani kavu ya mti.

“Anapaswa kuwa katika uwanja wa mieleka wa WWE na sio kanisani sehemu kubwa ya mazoezi yake ya viungo ameiga kutoka WWE,” Ndaire Peter aliandika.

“Hapa ni wakati kihalisia unashindwa kuigiza kama unazimia halafu yeye anachukua uamuzi wa kukulazimisha uzimie,” Nokilycious alisema.