Mtangazaji mkongwe wa KBC ahitaji msaada wa damu baada ya kugundulika na saratani

Watu wa kundi lolote la damu wameombwa kujitolea kutoa damu kwa Bi Kasavuli.

Muhtasari

•Bi Kasavuli amelazwa katika KNH baada ya kugundulika kuwa na saratani ya shingo ya kizazi (Cervical Cancer).

•Watu pia wameombwa kumkumbuka mtangazaji huyo katika maombi yao na pia kutoa msaada wa aina nyingine yoyote.

Mtangazaji Catherine Kasavuli
Image: HISANI

Mtangazaji mkongwe wa KBC Catherine Kasavuli anaendelea kupokea matibabu maalum katika hospitali ya Kenyatta baada ya kulazwa.

Gwiji huyo wa utangazaji wa habari amelazwa katika hospitali hiyo baada ya kugundulika kuwa na saratani ya shingo ya kizazi (Cervical Cancer).

Katika jitihada za kurejesha afya ya Bi Kasavuli, ombi la damu limetolewa na watu wa kundi lolote la damu wameombwa kujitolea.

"Wapendwa marafiki, wafanyakazi wenza na watu wenye nia njema. Mwenzetu mpendwa Catherine Kasavuli amelazwa katika Mrengo wa Kibinafsi wa KNH. Kwa wale wanaoweza, anahitaji kuwekwa damu mishipani haraka," taarifa iliyofikia Radio Jambo ilisoma.

Watu pia wameombwa kumkumbuka mtangazaji huyo katika maombi yao na pia kutoa msaada wa aina nyingine yoyote.

Kituo cha Runinga cha Kitaifa cha KBC Channel 1 pia kimefanya ombi la msaada wa damu kwa ajili kwa mfanyakazi huyo wake kupitia kurasa rasmi za mitandao ya kijamii.

"Mtangazaji mkongwe Catherine Kasavuli amelazwa katika Hospitali ya KNH, Mrengo wa Kibinafsi baada ya kugundulika kuwa na saratani ya shingo ya kizazi. Kundi lolote la damu litafanya," taarifa ya KBC ilisoma.

Kasavuli ,60, alikuwa mtangazaji wa kwanza wa habari wa kike nchini Kenya na amewahi kufanya kazi katika vituo kadhaa maarufu vya televisheni vikiwemo  KBC, Citizen TV na KTN.