"Nimechoka!" Akothee alazimika kupumzika kitandani, aeleza kwa nini

Mwimbaji huyo alilalamika kwamba anihisi kuchoka sana na hivyo kulazimika kupumzika.

Muhtasari

•Akothee aliweka wazi kuwa hatapokea simu katika kipindi hicho na pia akaomba asiitwe kwa mikutano yoyote.

•"Leo nimefanya na nimemaliza. Acheni nichukue mapumziko ya siku tano. Nitarudi. Nawapenda," alisema.

Mwanamuziki Akothee
Mwanamuziki Akothee
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji na mjasiriamali mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee ametangaza kuwa atachukua mapumziko ya kitandani ya siku tano.

Jumapili jioni, mama huyo wa watoto watano alilalamika kwamba anihisi kuchoka sana na hivyo kulazimika kupumzika.

"Nimekuwa nikifanya mengi na ninahisi uchovu, kwa hivyo kwa upole nitakuwa na mapumziko ya kitandani ya lazima ya siku tano," alitangaza kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Aliweka wazi kuwa hatapokea simu katika kipindi hicho cha mapumziko na pia akaomba asiitwe kwa mikutano yoyote.

Alieleza kwamba alichoka akizunguka zunguka kukusanya vifaa vya ujenzi wa shule yake ya, Akothee Foundation Academy.

"Leo nimefanya na nimemaliza. Acheni nichukue mapumziko ya siku tano. Nitarudi. Nawapenda," alisema.

Siku za hivi majuzi mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 42 amekuwa akijihusisha katika shughuli nyingi pamoja na mpenzi wake, Bw Omosh.

Hivi majuzi pia alikarabati barabara moja ya umma inayopitia karibu na nyumbani kwake katika eneo la Rongo, kaunti ya Migori.

Kwa utani, mwimbaji huyo alidai kufidiwa na serikali ya Migori baada ya kutumia pesa zake kukarabati barabara hiyo.

"Barabara hii ni ya serikali, imekuwa haipitiki wakati wa mvua kubwa, watu wangu wote kutoka eneo hili waliikwepa na kutafuta njia mbadala, wengine waliegesha magari na kutumia pikipiki kwenye njia mbadala," alisema.

Alijivunia kuwa sasa barabara hiyo inaweza kupitika kwa urahisi angalau na magari yanaweza kuitumia bila shida nyingi.

"Serikali ya Kaunti ya Migori inafaa kunirudishia pesa zangu mara tu bajeti ya barabara itakapokamilika," alisema.

Mara nyingi amedokeza kuwa mpenzi wake mzungu amekuwa akimuunga mkono sana katika kazi na biashara zake.

Siku chache zilizopita alithibitisha kuwa uchapakazi wa mpenzi wake mpya ndio uliomvutia ajitose kwenye mahusiano naye.

Kwenye Instagram, Akothee alichapisha video iliyomwonyesha mpenzi huyo wake mzungu akifanya kazi mida ya majogoo.

"Omosh wangu, mwendo wa saa kumi na moja  asubuhi, sasa mnajua lugha yangu ya mapenzi," aliandika chini ya video hiyo.