Mtu yeyote anavalia mkanda wa mkononi, ndoa yake ina tatizo - Pastor Ezekiel

Mchungaji huyo alizidi kuwauliza baadhi ya waumini waliokuwa na mikanda hiyo ambao walikubali ndoa zao zina nyufa.

Muhtasari

• "Ukiuliza mtu yeyote ako nayo, muulize tu awe mkweli kama ndoani kuko sawa,” mchungaji huyo alihubiri.

Mchungaji aonya dhidi ya uvaaji wa mikanda ya mkononi
Mchungaji aonya dhidi ya uvaaji wa mikanda ya mkononi
Image: Jiji, Alibaba, Facebook

Mchungaji mmoja nchini Kenya kwa jina Ezekiel amezua mjadala mkali mitandaoni baada ya kudai kuwa mikanda ya mikononi inaharibu ndoa pakubwa nchini na kote ulimwenguni.

Mchungaji huyo katika klipu inayosambazwa inauonesha akiwauliza waumini wanaoonekana na mikanda hiyo mbali mbali ambao wengi wanajutia kuwa hawakuwa wanajua kama ndicho chanzo cha kuvurugika kwa ndoa na matatizo ya kujirudia kwenye uhusiano.

Mchungaji Ezekiel alianza kuwauliza waumini mmoja baada ya mwingine na kuwataka pia waulize mtu yeyote wanayemuona na mkanda huo unaovaliwa mkononi kama saa kama kweli ndoa zao ziko imara.

Idadi kubwa ya wakenya wamekumbatia kuvalia mikanda hiyo yenye nembo ya bendera ya nchi kwenye mikono yao na hao ndio wamejipata katika gumzo kubwa.

“Mwanaume yeyote anayevalia huo mkanda wa mkononi, huwa ndoa yake inamsumbua. Yeyote hata kama ni mheshimiwa na ako na hiyo ribbon, ndoa yake ina matatizo ni kutangaza hawatangazi. Ukiuliza mtu yeyote ako nayo, muulize tu awe mkweli kama ndoani kuko sawa,” mchungaji huyo alihubiri huku waumini wakiwa wameshika tama wasiweze kuamini wanachokisikia.

Mwanadada mmoja aliyeulizwa na mchungaji huyo kuhusu ndoa yake alitoa majibu ya kustaajabisha ambapo alisema ndoa yeke ni ya vichekesho.

Mchungaji Ezekiel alitetea mahubiri yake akisema kuwa hakuna kitu amabcho mtu anaweza valia mwilini mwake na kisimpe mwelekeo wa maisha yake jinsi yatakavyokuwa.

“Hata mtu wa kuvaa miwani huwa ana shida ya macho. Vitu vingi sana vinakuja na sababu zao. Hata dera liko na sababu na maana yake,” mchungaji Ezekiel alisema.