Daddy Owen hatimaye afunguka kwa nini alimkataa Pritty Vishy

"Sifa zingine ako sawa. Kama hajalelewa ushago hapana," alisema.

Muhtasari

•Owen alisema kuzaliwa na kulelewa mjini kwa kipusa huyo ambaye hujitambulisha kama 'Kienyeji Pro Max' kulimuondoa kwenye orodha ya wanawake waliohitimu kuwa mkewe.

•Mwanamuziki huyo mkongwe alisisitiza kuwa mwanadada atakayekuwa mke wake ni sharti awe amelelewa kijijini.

Daddy Owen na Pritty Vishy
Image: INSTAGRAM

Mwimbaji wa nyimbo za injili Owen Mwatia almaarufu Daddy Owen ameweka wazi kwamba aliyekuwa mpenzi wa mwanamuziki Stivo Simple Boy, Purity Vishenwa almaarufu Pritty Vishy hakufikia sifa za kuwa mke wake.

Katika mahojiano na Plug TV, Owen alisema kuzaliwa na kulelewa mjini kwa kipusa huyo ambaye hujitambulisha kama 'Kienyeji Pro Max' kulimuondoa kwenye orodha ya wanawake waliohitimu kuwa mkewe.

"Pritty Vishy hajalelewa ushago (kijijini). Hiyo ndio inamuondoa. Sifa zingine ako sawa. Kama hajalelewa ushago hapana," alisema.

Mwanamuziki huyo mkongwe alisisitiza kuwa mwanadada atakayekuwa mke wake ni sharti awe amelelewa kijijini.

Siku chache zilizopita Pritty Vishy alijitolea kuwa mke wa  Daddy Owen baada ya mwimbaji huyo kudaiwa anatafuta mwanamke 'kienyeji'.

Kipusa huyo mwenye umri wa miaka 21 alitoa ombi kwa watu wanaoweza kumfikia msanii huyo kumwambia kwamba yupo radhi kuwa mke wake kwani tayari kigezo cha kuwa kienyeji tayari anacho.

"Si mtu amwambie Daddy Owen kwa niaba yangu kuwa nipo singo na bila vipodozi mimi ni mweusi wa asili. Mimi si rangi ya mkorogo kwa sababu sijui mtu anakuwa mkorogo aje. Pia napenda maombi sana, ifikie Daddy Owen," alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Katika jibu lake, Owen alimwambia Vishy kuwa anapaswa kusubiri kwa kuwa foleni ni ndefu sana na bado hajafikiwa.

"Huyu mwambieni line ni ndeefu,hajafikiwa bado..lakini kama marathon tutazawadi kila mmoja atakaye vuka laini," Alisema.

Vishy alionekana kughadhabishwa na jibu la mwanamuziki huyo na kukinzana na kauli yake ya awali kuwa alitaka kuwa mke wake.

“Nilikuwa namtaka lakini sasa ni kama atavuka upande wa Uganda, ni mwanaume yupi ambaye anataka kuwa na ufisadi? Nasikia hataki mwanamke ambaye yuko kwenye mtandao wa TikTok na anayeongea Kizungu kingi,” Vishy alisema.

Daddy Owen hata hivyo sasa ameweka wazi kuwa bado hajajitosa kwenye pilka pilka za kutafuta mwanamke wa kuchumbia na kuoa.

"Mimi ni mwanaume, siwezi kutangaza kuwa natafuta mwanamke. Mimi ni simba, nikitaka mwanamke nitaenda huko nje na niwinde," alisema.

Awali alikuwa amesema kwamba mama yake amekuwa akimpa shinikizo la kutafuta mwanamke wa kuwa akitembea naye nyumbani.