Akothee hatimaye arejea baada kuchukua mapumziko kutokana na uchovu

Mwimbaji huyo alichapisha video inayomuonyesha mpenzi wake mzungu akipapasa miguu yake.

Muhtasari

• Akothee alilalamika kwamba anahisi kuchoka sana, jambo ambalo lilimlazimu kupumzika kwa siku tano.

•"Omosh atajua ameoa mjaluo. Omosh atajua hajui, kuoa mjaluo ni gharama," alisema.

Akothee
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji na mjasiriamali mashuhuri Akothee amerejea tena mitandaoni, takbriban siku tano baada ya  kutangaza kwamba atachukua mapumziko mafupi.

Siku ya Jumapili jioni, mama huyo wa watoto watano alilalamika kwamba anahisi kuchoka sana, jambo ambalo lilimlazimu kupumzika kwa siku tano.

"Nimekuwa nikifanya mengi na ninahisi uchovu, kwa hivyo kwa upole nitakuwa na mapumziko ya kitandani ya lazima ya siku tano," alisema.

Mwanamuziki huyo aliweka wazi kuwa hangepokea simu katika kipindi hicho cha mapumziko na pia akaomba asiitwe kwa mikutano yoyote.

Alieleza kwamba alichoka akizunguka zunguka kukusanya vifaa vya ujenzi wa shule yake ya, Akothee Foundation Academy.

"Leo nimefanya na nimemaliza. Acheni nichukue mapumziko ya siku tano. Nitarudi. Nawapenda," alisema.

Akothee aliendelea kuchukua mapumziko kama alivyotangazwa na amekosekana kwenye mitandao ya kijamii katika siku kadhaa zilizopita. 

Alhamisi jioni alidokeza kurejea kwake kwa kuchapisha video fupi inayomuonyesha  mpenzi wake mzungu akipapasa miguu yake.

Ijumaa asubuhi alichapisha video zingine zikimuonyesha akimtayarishia mpenziwe kifungua kinywa na akiandamana naye kusimamia mjengo.

"Omosh atajua ameoa mjaluo. Omosh atajua hajui, kuoa mjaluo ni gharama," aliandika chini ya video zinazoonyesha akimkabidhi mpenziwe uji na viazi vitamu.

Siku za hivi majuzi mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 42 amekuwa akijihusisha katika shughuli nyingi pamoja na mpenzi wake, Bw Omosh.

Mara nyingi amedokeza kuwa mpenzi wake mzungu amekuwa akimuunga mkono sana katika kazi na biashara zake.

Siku chache zilizopita alithibitisha kuwa uchapakazi wa mpenzi wake mpya ndio uliomvutia ajitose kwenye mahusiano naye.

"Habari za asubuhi wafalme na malkia. Mnaona sababu kwa nini Bwana Omondi aliuteka moyo wangu. Huwa ameamka kabla ya saa kumi na moja asubuhi, aah Mungu huyu💪💪💪💪.. na ndio maana nilimpatia jina Omondi," aliandika chini ya picha iliyomuonyesha akiwa na mpenzi wake wakitembelea shamba lake. Wawili hao walionekana wakizunguka shamba hilo kubwa na kuzungumza na wafanyakazi.

Mama huyo wa watoto watano pia alidokeza kuwa mpenzi wake mpya ni tajiri mkubwa. Alijigamba kuwa mahusiano yake mapya yamefanya akawa mwenye furaha zaidi na kuongeza urembo wake.

"Lakini huyu mzungu wangu amefanya nimekuwa mrembo na mwenye furaha sana, haki pesa wewe ni sabuni ya mapenzi. Hakuna kitu tamu kama kuchumbiana na mwanaume ako na pesa zake. Tamuuuu," alisema.

Akothee alitangaza mahusiano yake mapya mwezi uliopita baada ya kumficha mpenziwe hadharani kwa muda mrefu.