Vera Sidika afichua tarehe na mipango ya harusi yake na Brown Mauzo

Pia alidokeza mipango ya kupata mtoto mwingine na mwimbaji huyo katika siku za usoni.

Muhtasari

•"Mimi ni mtu anayependa ukamilifu kwa hivyo ningetaka kuchukua wakati kupanga kila ktu kwa ukamilifu," alisema,

•Vera aliwahi kuweka wazi kuwa yupo kwenye ndoa halali na mwimbaji huyo kutoka Pwani.

Vera Sidika, Brown Mauzo na binti yao Asia Brown.
Image: INSTAGRAM// VERA SIDIKA

Mwanasoshalaiti mashuhuri  wa Kenya  Vera Sidika amefichua mipango ya kufanya harusi ya kanisa na mchumba wake Brown Mauzo.

Siku ya Jumamosi, mama huyo wa binti mmoja aliwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye Instagram ambapo alifunguka kuhusu masuala mbalimbali ya maisha yake yakiwemo mahusiano.

"Je, umewahi kufikiria kufanya harusi ya kanisa?" mtumizi mmoja wa Instagram aliuliza.

Katika jibu lake, mwanasoshalaiti huyo mwenye umri wa miaka 33 alifichua kwamba yeye na mumewe wanapaga kufunga pingu za maisha  kanisani mwishoni mwa mwaka ujao ama mwanzoni mwa mwaka wa 2024.

"Mimi ni mtu anayependa ukamilifu kwa hivyo ningetaka kuchukua wakati kupanga kila ktu kwa ukamilifu," alisema,

Katika kipindi hicho, Vera alijibu swali la tofauti ya umri na kusisitiza kuwa mumewe anaamzidi umri kwa miaka miwili.

Pia alidokeza mipango ya kupata mtoto mwingine na mwimbaji huyo katika siku za usoni.

"Unampa Asia ndugu mdogo lini?" shabiki aliuliza.

Vera alijibu, "Labda 2024. Lakini Mungu ndiye anayejua vizuri. Kwa sasa mimi naangazia kazi na miradi mingi."

Mara kadhaa katika siku za nyuma Vera aliwahi kuweka wazi kuwa yupo kwenye ndoa halali na mwimbaji huyo kutoka Pwani.

Katika mahojiano na mtangazaji Masssawe Japanni mwezi uliopita, Mwanasoshalaiti huyo alifichua kuwa anafurahia ndoa yake na Mauzo ambayo sasa imedumu kwa takriban miaka miwili unusu.

Vera alisema kwamba yeye na Mauzo walikuwa marafiki kwa miezi kadhaa kabla ya kuanza kuchumbiana.

Baada ya kuwa marafiki na kujuana kwa muda, aligundua kuwa mwimbaji huyo ni mwanaume tofauti.

"Niliona ni mtu tofauti. Brown hata hajawahi kunywa pombe. Tulikuwa tunapigiana simu na kuongea kutoka  saa  tatu usiku  mpaka saa kumi na moja asubuhi. Tulikuwa marafiki. Tulikuwa wazi sana," alisema.

Mama huyo wa binti mmoja hata hivyo alikiri kuwa hakutazamia kuchumbiana na mtu mwingine maarufu baada ya mahusiano yake na  mwanamuziki Otile Brown kugonga mwamba mwakani 2018.