"Ndoa si ulaghai!" Mwimbaji Esther Wahome aisifu ndoa yake nzuri ya miaka 26

Esther alikanusha madai kwamba ndoa nyingi za watu mashuhuri hazidumu.

Muhtasari

•Alizungumza sana kuhusu kuwa na familia nzuri, akisema anapendelea kuwaficha wanafamilia wake kutoka hadharani.

•"Familia yangu ni ya kibinafsi na ninapenda kuchagua vita vyangu, lakini nina ndoa nzuri," alisema.

Image: FACEBOOK// ESTHER WAHOME

Mwimbaji mkongwe wa nyimbo za Injili Esther Wahome amewahimiza watu wasio na wapenzi kukumbatia ndoa.

Msanii huyo ambaye muziki wake uliwahi kuchezwa katika karibu kila stesheni ya runinga na redio zilizopo, alitoa wito kwa watu waache kuita ndoa ‘ulaghai’.

“Nimeolewa kwa miaka 26 na mwanamume mzuri ambaye kila siku ananisukuma niwe vile Mungu anataka niwe bila kunilazimisha niwe kwenye macho ya umma,” alisema.

Mama huyo wa watoto watatu alisema watoto wake wote ni watu wazima.

Mzaliwa wake wa kwanza amekamilisha masomo ya chuo kikuu, mzaliwa wa mwisho anakaribia kuingia shule ya upili, wakati mzaliwa wa pili tayari yuko katika shule ya upili.

Alizungumza sana kuhusu kuwa na familia nzuri, akisema anapendelea kuwaficha wanafamilia wake kutoka hadharani.

"Siwaweki mitandaoni isipokuwa ambaye alimaliza chuo kikuu. Aliweka mtandaoni tangu alipotimiza umri wa zaidi ya miaka 18," alisema na kuongeza kuwa anasubiri watoto wake wafanye maamuzi yao wenyewe.

"Familia yangu ni ya kibinafsi na ninapenda kuchagua vita vyangu, lakini nina ndoa nzuri," alisema.

Esther alikanusha madai kwamba ndoa nyingi za watu mashuhuri hazidumu.

Aliwahimiza watu kuzingatia waliofanikiwa.

“Angalia maisha yangu, tuanze kuzungumzia ndoa zenye mafanikio tulizonazo kwani ni nyingi kwenye tasnia,” alisema.

"Mtu kama Sarah K ana zaidi ya miaka 30 kwenye ndoa, na mwimbaji Jemimah Thiong'o ana karibu miaka 40 kwenye ndoa.

Hata katika tasnia ya muziki wa burudani, tunao, Wahu na Nameless, kwa hivyo ndoa sio ulaghai kwa maoni yangu."

Kuhusu kwa nini baadhi ya wasanii wa nyimbo za injili waliacha tasnia hiyo, Esther alisema ni watumishi wa kweli wa Mungu pekee wanaodumu kwenye tasnia hiyo.

“Ukiwa mkweli, utaokoka na utakuwa baraka kwa sababu kuna kizazi unatumikia,” alisema.

"Ikiwa ni kwa ajili ya pesa na kiki, hautadumu kwani kuna nguvu zinazohitaji mtu kuwa mkweli na mwenye maombi wakati wa kufanya muziki wa injili. Utafanya kibao na kuacha tasnia na kutuacha sisi ambao tunatumikia kwa kweli."

Mama huyo wa watoto watatu pia alifunguka kuhusu hadithi za uponyaji, urejesho na matumaini kutoka kwa watu ambao wamesikiliza baadhi ya nyimbo zake kwa miaka mingi.

“Nimekutana na walevi wanasema wimbo wangu wa ‘Kuna Dawa’ uliwatoa machozi wakiwa vilabuni, sijui kwanini,” alisema.

"Kuna mtu katika Barabara ya Jogoo ambaye pia alisema alisikiliza 'Kuna Dawa' na akapona."