Samidoh azungumzia kumtumia promota wake mrembo kumuumiza mkewe

Mwimbaji huyo ameendelea kuwachanganya watu kuhusu uhusiano wake halisi na Bernice.

Muhtasari

•Hivi majuzi,  mwanamuziki huyo alichapisha video iliyomuonyesha akifurahia muda mzuri na Bernice. 

•"Heshimu mama watoto kaka," mtumizi mmoja wa Tiktok alimwambia mwimbaji huyo.

Samidoh na Bernice Saroni
Image: HISANI

Staa wa Mugithi Samuel Muchoki almaarufu Samidoh amekuwa gumzo mitandaoni katika siku za hivi majuzi huku akidaiwa kuwa na uhusiano ya kimapenzi na promota wake Bernice Saroni.

Siku za hivi majuzi, mwimbaji na mpiga gitaa huyo mahiri ambaye kwa sasa yuko kwenye ziara ya muziki nchini Marekani ameonekana kwenye picha na video akifurahia muda na mwanadada huyo mrembo mwenye umbo nzuri.

Huku tetesi za mahusiano na Bernice zikiendelea, Samidoh bado hajajitokeza kuthibitisha au kukanusha madai hayo. Badala yake ameendelea kuwachanganya wanamitandao kuhusu uhusiano wake promota huyo.

Hivi majuzi,  mwanamuziki huyo alichapisha video iliyomuonyesha akifurahia muda mzuri na Bernice. Katika video hiyo, wawili hao walijawa na tabasamu usoni huku wakiimba wimbo wa Kikuyu  pamoja.

Kama kawaida, wanamitandao walimiminika chini ya chapisho hilo na kutoa maoni tofauti kuhusu video hiyo.

"Heshimu mama watoto kaka," mtumizi mmoja wa Tiktok alimwambia mwimbaji huyo.

Samidoh alijibu, " Toa maoni kuhusu mambo ambayo unaelewa kaka. Vinginevyo, hiyo kiherehere pelekea bibi yako."

Staa huyo wa Mugithi pia aliwasuta wanamitandao wengine ambao walijaribu kumvuta Bernice kwenye ndoa yake na kudai kuwa alichapisha picha zake ili kumuumiza mkewe. 

Baadhi ya wanamitandao hata hivyo waliibua madai kuwa mwanadada huyo ni mwanafamilia wa Samidoh na kusema wanajua walichokuwa wakifanya.

Katika ukurasa wake wa Facebook, Samidoh pia alichapisha picha yake na promota huyo na wanamitandao wakamiminika kutoa maoni.

"Wee ukiona mwanaume anapost mwanadada ujue anajaribu kuumiza mtu mwingine . Samidoh ushauri wangu kwako ni bibi yako ndiye atakufulia nguo siku ambayo utakuwa na shida, wanasoshalaiti wapo hapo kwa wakati mzuri tu," mtumizi mmoja wa Facebook alimwambia katika sehemu ya maoni.

Alijibu, "Hiyo ni hoja ya kijinga. Unahitaji kuchimba zaidi kwa maelezo." 

Hivi majuzi mzazi mwenza wa Samidoh, Karen Nyamu alidaiwa kuzozana na Bernice kuhusu mwimbaji huyo.

Karen alipoulizwa ikiwa anapigania mzazi huyo mwenzake alisema, ""Simpiganii, lakini anastahili kupiganiwa,"