Zari atembelea kaburi la aliyekuwa mumewe Ivan Ssemwanga akiwa na mpenziwe Shakib (+video)

Bw Ivan Ssemwanga aliaga dunia mnamo Mei 25, 2017 baada ya kuugua.

Muhtasari

•Zari alikuwa ameandamana na watu wengine kadhaa akiwemo mpenzi wake wa sasa Shakib Cham Lutaaya wakati alipotembelea kaburi hilo.

•Wawili hao walikuwa kwenye ndoa kwa zaidi ya mwongo mmoja na kujaliwa watoto watatu pamoja kabla ya kutengana.

waliembelea kaburi la aliyekuwa mume wake Ivan Ssemwanga
Zari Hassan na mpenzi wake Shakib Cham waliembelea kaburi la aliyekuwa mume wake Ivan Ssemwanga
Image: HISANI

Mwanasosholaiti maarufu wa Uganda Zari Hassan hivi majuzi alitembelea kaburi la marehemu mume wake wa zamani Ivan Ssemwanga.

Zari alikuwa ameandamana na watu wengine kadhaa akiwemo mpenzi wake wa sasa Shakib Cham Lutaaya wakati alipotembelea kaburi hilo lililo katika kijiji cha Nakaliro, katika Mji wa Kayunga, nchini Uganda.

Alirekodi video fupi ikimuonyesha akiwa amekaa kwenye kaburi hilo la baba wa watoto wake watatu wa kwanza huku watu wengine ambao walikuwa wameandamana naye wakipumzika kuzunguka eneo hilo.

Hii sio mara ya kwanza kwa mama huyo wa watoto watano kutembelea eneo hilo. Zari amekuwa akienda pale mara kwa mara tangu mume huyo wake wa zamani alipoaga dunia mnamo Mei 25, 2017 baada ya kuugua.

Bw Ssemwanga, ambaye alikuwa mfanyibiashara tajika nchini Afrika Kusini alifariki katika hospitali ya Steve Biko Academic, jijini Pretoria, Afrika Kusini ambako alikuwa amekimbizwa akiwa katika hali mbaya.

Baadaye alizikwa kijijini kwao Nakaliro katika hafla ghali iliyohudhuriwa na watu maarufu na matajiri nchini Uganda na kwingineko ikiwa ni pamoja na wanamuziki Jose Chameleone, Bobi Wine, SK Mbuga na Weasel.

Kiasi kikubwa cha pesa na mvinyo ghali vilimwagwa ndani ya kaburi la mfanyibiashara huyo baada ya jeneza lake kuteremshwa. 

Ssemwanga ambaye alitambulika kama kiongozi wa Rich Gang nchini Uganda alifariki akiwa na umri wa miaka 39 na aliacha nyuma watoto watatu wa kiume ambao alikuwa amepata na mwanasoshalaiti Zari Hassan.

Wawili hao walikuwa kwenye ndoa kwa zaidi ya mwongo mmoja na kujaliwa watoto watatu pamoja kabla ya kutengana. Baadae Zari alijitosa kwenye mahusiano na Diamond na kupata watoto wengine wawili naye.

Hata hivyo alitengana na staa huyo wa Bongo mwaka wa 2018 akaenda kuendesha biashara zilizoachwa na Bw Ivan nchini Afrika Kusini. Kwa sasa anachumbiana na Shakib Lutaaya mwenye umri wa miaka 31.