"Nataka mtoto wa 6!" Bahati amwambia mkewe Diana Marua

Bahati alidokeza kuwa anatazamia kupata mtoto wa nne na Diana Marua mwezi Oktoba.

Muhtasari

•Bahati alifichua kwamba mke wake anatazamia kuwa na tumbo tambarare ifikapo mwisho wa mwaka huu.

•Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 30 alidokeza kuwa anataka wapate mtoto mwingine ifikapo mwisho wa 2023.

Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA

Mwimbaji Kelvin Kioko almaarufu Bahati alishiriki mazungumzo na mke wake Diana Marua ambapo walijadili malengo yao ya 2023.

Wanandoa hao walichapisha kijisehemu cha video ya mazungumzo yao kwenye mtandao wa Instagram siku ya Jumatano.

Katika video hiyo, Bahati alifichua kwamba mke wake anatazamia kuwa na tumbo tambarare ifikapo mwisho wa mwaka huu.

"Mambo matatu ambayo mke wangu anataka kutimiza mwaka wa 2023, nambari moja, tumbo tambarare.. mke wangu anakula kama fundi," msanii huyo alisema na Diana Marua akakubaliana naye kwa yote.

Katika kauli kinzani, mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 30 alidokeza kuwa anataka wapate mtoto mwingine ifikapo mwisho wa mwaka.

"Mafanikio yangu mengine ninayotaka kutimiza 2023, nataka kuwa na mtoto wa sita," alisema na kuendelea kusherehekea mbele ya mkewe ambaye alionekana wazi kutofurahishwa na lengo hilo lake.

Bahati zaidi alidokeza kwamba anatazamia kuwa na mtoto wa nne na Diana Marua mwezi wa Oktoba.

"Nipewe haki yangu nisipewe? Tupatane hospitalini Oktoba kama hisabati yangu inaingiana,"

Diana Marua pia alifichua kwamba mwaka huu analenga kufikisha wafuasi zaidi ya  milioni moja kwenye mtandao wa YouTube na kuwa mwanamke wa kwanza Mwafrika kupata kijisahani cha dhahabu cha YouTube.

Kukiri kwa Bahati kuhusu kutaka mtoto wa sita kunakuja miezi michache tu baada ya mkewe kujifungua mtoto wao wa 3 pamoja.

Wanandoa hao walibarikiwa na mtoto wa kike, Malkia Bahati  mnamo Novemba 1, 2022.

Akitangaza habari hizo kwenye Instagram, Bahati aliweka picha yake akiwa amemshikilia mtoto huyo karibu na kifua chake na kuandika, "Malaika Nyambura Bahati alizaliwa Novemba 1, 2022, utukufu kwa Yesu!!! @malaika_bahati."

Wawili hao wana watoto wengine wawili pamoja Heaven Gift Bahati na Majesty Bahati.

Bahati ana mtoto mwingine mmoja na aliyekuwa mpenzi wake, Yvette Obura. Mueni Bahati mwenye umri wa miaka saba ndiye mtoto wa mwimbaji huyo.

Pia ana mtoto mwingine, Morgan Bahati, ambaye alimchukua kutoka kwa nyumba ya watoto na kumlea kama wake.