Mwanamuziki mashuhuri Kelvin Kioko almaarufu Bahati hatimaye amefunguka kuhusu ukimya wake punde baada ya uchaguzi wa Agosti 9, 2022.
Mwaka jana, msanii huyo mwenye umri wa miaka 30 alijitosa katika siasa na alikuwa mmoja wa wagombea kiti cha ubunge wa Mathare akiwania kwa tikiti ya chama cha Jubilee. Hata hivyo, alipoteza uchaguzi huyo kwa mgombea wa ODM Anthony Oluoch.
Baada ya uchaguzi huo, Bahati alitoweka kwenye vyombo vya habari na mitandao yote ya kijamii huku Wakenya wengi wakikisia kuwa alikuwa amekumbwa na msongo wa mawazo kwa kutofanikiwa kupata ushindi katika uchaguzi.
Mwanamuziki huyo hata hivyo ameweka wazi kwamba alichukua mapumziko kutoka kwa umma ili kuangazia muziki wake.
"Nilikuwa nimejifungia tu kwenye Studio ya Nyumbani nikitengeneza Sauti Bora za Muziki kwa ajili yenu mashabiki wangu tangu siku ya kwanza," alisema kupitia ukuraa wake wa mtandao wa nstagram.
Alibainisha kuwa ilikuwa ni mapumziko ya mitandao ya kijamii ya kwanza aliyokuwa akichukua katika kipindi cha miaka kumi
"Naapa nasikiliza nyimbo ambazo nimepanga kuachia mwaka huu wa 2023 ata sina usingizi. Walai sikujua Bahati ni mkali hivii," alijigamba.
Bahati alidokeza kuwa umahiri wake katika muziki umeongezeka huku akifanya mzaha kuwa huenda imechangiwa na kuibiwa kwa kura zake.
Katika uchaguzi wa mwaka jana, Bahati aliibuka wa tatu katika kinyang’anyiro cha ubunge wa Mathare huku Anthony Oluoch wa ODM akichukua ushindi. Billian Ojiwa ambaye aliwania kwa tiketi ya UDA alimaliza katika nafasi ya pili.
Hilo lilikuwa ni jaribio la Bahati la kwanza kuwania kiti cha kisiasa nchini Kenya.
Baada ya kuvunjwa moyo katika uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkubwa, mwanamuziki huyo alizama kwenye ukimya mrefu.
Hatimaye aliibuka tena hadharani baada ya takriban miezi miwili kwa wimbo 'Mambo ya Mhesh’ ambao alipakia kwenye YouTube.