(Video) Dereva na Makanga wake warushiana ngumi katikati ya barabara Nairobi

Dereva alijaribu kumtupia teke makanga lakini kwa bahati mbaya akaanguka chini.

Muhtasari

• Wawili hao walionekana wakirushiana ngumi katika barabara moja jijini Nairobi.

Shirika lisilo la kiserikali la kuhamasisha kuhusu usalama barabarani la Sikika Road Safety limepakia video ya dereva na kondakta wake wakipapurana vikali katikati ya barabara.

Video hiyo ambayo ilionekana kuchukuliwa katika barabara moja jijini Nairobi, inaonesha dereva wa matatu ya kubeba abiria 14 akisukumana vikali na mwanamume mwingine mwenye sare ya makanga.

Katika tukio hilo, dereva huyo ambaye ni mzee kidogo alionekana kama anamkataza makanga mwenye muonekano wa kijana dhidi ya kutoingia kwenye mlango wa kuingilia abiria wa matatu hiyo, lakini makanga naye alionekana kusisitiza kutaka kuingia.

Hapo ndipo dereva alipandwa na jazba na kumtupia kofi makanga lakini akalikwepa kofi hilo kabla ya kuanza kutoroka na dereva kumfuata nyuma mbio akiwa na lengo la kumtia japo kofi moja.

Wawili hao walifukuzana hadi kando ya barabara ambapo Dereva baada ya kushindwa kumfikia kwa mikono makanga, aliamua kuajiri mguu wake kwa kazi ya kumpiga teke makanga.

Kwa bahati mbaya makanga alikwepa pia lile teke kufanya dereva yule mzee kuanguka chini kwa kishindi huku watu wakicheka na makanga yule naye akitoroka kwa kicheko kikubwa.

Sikika hawakuweza kutoa maelezo zaidi kuhusu video hiyo ilitokea katika barabara gani au hata kusimulia kiini cha vita hiyo ya dereva na makanga wake, ila walisema tu waliamua kulinyamazia hilo.