"Natafuta mpenzi" Aliyekuwa mpenzi wa Stivo Simple Boy, Pritty Vishy ajitenga na LGBTQ

Vishy alifichua kuwa anaendelea kutafuta mpenzi wa kumridhi Simple Boy.

Muhtasari

•Huku akiwajibu wakosoaji wake kwenye Instagram, Vishy aliweka wazi kuwa hajajiunga na jamii ya wapenzi wa jinsia moja. (LGBTQ).

•"Napenda wanaume. Kwa hivyo acheni kueneza uvumi ama mnazosema ni habari naomba," alisema. 

Pritty Vishy
Image: INSTGRAM// PRITTY VISHY

Aliyekuwa mpenzi wa mwimbaji Stivo Simple Boy, Purity Vishenwa almaarufu Pritty Vishy amepuuzilia mbali madai kuwa  ni msagaji.

Huku akiwajibu wakosoaji wake kwenye Instagram, Vishy aliweka wazi kuwa hajajiunga na jamii ya wapenzi wa jinsia moja. (LGBTQ)

"Kwa hivyo leo nitakuwa mkweli na ninyi nyote, niko sawa na muache kusema kwamba nilijiunga na elijibitikiu!" alisema.

Licha ya kukana jamii ya LGBTQ, muunda maudhui huyo aliweka wazi kwamba hakuna ubaya kuwa mwanachama wao.

Pia alifichua kuwa anaendelea kutafuta mpenzi wa kumridhi Simple Boy baada ya kutengana na msanii huyo mwaka jana.

"Napenda wanaume. Kwa hivyo acheni kueneza uvumi ama mnazosema ni habari naomba," alisema. 

Haya yanajiri siku chache tu baada ya kidosho huyo mwenye umri wa miaka 21 kuwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha Maswali na Majibu kwenye Instagram ambapo alishinikizwa kuzungumzia madai hayo.

Katika kipindi hicho cha wiki iliyopita, wanamitandao walichukua fursa kumhoji mtumbuizaji huyo juu ya masuala mbalimbali yanayohusu maisha yake kuanzia masuala ya kibinafsi, mahusiano na mafanikio yake.

Mfuasi wake mmoja alimtaka afafanue kuhusu madai ya usagaji ambayo yamewahi kumkabili hapo awali.

"Je, Wewe ni msagaji? Kama ndiyo au hapana toa maelezo kwanini?" Shabiki alihoji.

Vishy alijibu, "Kama ndiyo au hapana siwezi kujieleza rafiki yangu."

Madai kwamba Vishy huenda kwa kiasi fulani ni msagaji yalichimbuka mwishoni mwa mwaka jana baada ya kuonekana akijivinjari na kubusu na rafiki yake mwanamke.

Mwezi Desemba mwaka jana, Pritty Vishy alizua gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuonekana akijivinjari na TikToker Becky Akinyi kwa njia ya kimahaba. Wawili hao walifurahiya muda pamoja kwenye eneo la burudani na kuchapisha baadhi ya matukio kwenye kurasa zao za Instagram.

Marafiki hao pia walishirikisha mashabiki wao katika kipindi cha moja kwa moja ambapo walionekana wakibusu mara kadhaa kwenye midomo huku wakibugia vinywaji. Wawili hao walionekana kuwa kwenye klabu.

Wanamitandao walitoa maoni chini ya video ya wawili hao waliibua maswali mengi wakitaka kufahamu uhalisi wa uhasiano wao.