Kajala aweka wazi sifa anayotafuta kwa mpenzi mpya atakayemrithi Harmonize

Mpenzi huyo wa zamani wa Harmonize amedokeza kwamba yupo tayari kujitosa kwenye mahusiano mapya.

Muhtasari

•Kajala alitangaza kutengana na Harmonize  mwezi Desemba baada ya kuchumbiana naye  kwa takriban miezi saba. 

•Muigizaji huyo amesema anataka mtu anayesherehekea siku ya kuzaliwa karibu wakati sawa wa mwaka naye.

Kajala na Harmonize wakati mahaba yao yalikuwa yamenoga
Image: HISANI

Muigizaji  mashuhuri Frida Kajala Masanja amedokeza kwamba yupo tayari kujitosa kwenye mahusiano mapya, takriban miezi miwili baada ya kutengana na bosi wa Kondegang, Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize.

Kajala alitangaza kuvunjika kwa mahusiano yake na Harmonize mapema mwezi Desemba baada ya kuchumbiana naye  kwa takriban miezi saba. Wawili hao walikuwa wamerudiana Aprili baada ya Harmonize kuomba msamaha

Mama huyo wa binti mmoja ameweka wazi kwamba sasa yuko tayari kujaribu mahusiano na mtu wa ishara sawa ya zodiac na yeye, kumaanisha mtu anayesherehekea siku ya kuzaliwa karibu wakati sawa wa mwaka naye.

"Nataka kuchumbiana na ishara yangu. Nataka nione kama tutakuwa na tabia sawa na kama tutadumu," alisema kwenye Instagram.

Wakati akitangaza kutengana na Harmonize mwishoni mwa mwaka jana, Kajala aliweka wazi kwamba alikuwa tayari kupiga hatua nyingine baada ya mahusiano yao ya miezi michache kugonga mwamba.

Ingawa hakufichua kilichowatenganisha, aliweka wazi kwamba hakubeba kinyongo chochote dhidi ya mwimbaji huyo.

"Mimi kama mwanamke na binadamu nimeumbwa kupenda na kusamehe pia, ila kwenye hili nastahili kuchekwa, nastahili kubezwa na kudharauliwa pia. Sipo hapa kujitetea wala kutia huruma ni kweli nilifanya makosa na nimeyagundua makosa yangu, mimi siyo mkamilifu," Kajala alisema mwezi Desemba.

Takriban wiki mbili zilizopita,Harmonize alidokeza kuwa mzazi wake alimtahadharisha kuhusu mpenzi huyo wake wa zamani..

Katika ufichuzi aliofanya kama ushauri, bosi huyo wa Kondegang aliwashauri watu kuwapa sikio wazazi wao kila siku. Alibainisha kuwa wazazi huwa na jicho maalum la kuwasaidia kuona mambo yaliyofichwa ndani ya mtu.

"Msikilize mama!! Awe ni mama yako mzazi au mama wa mwenzio, baba yako ama wa mwenzio.. wazazi wanakuwanga na jicho la mbali sana. Mzazi ni rahisi kugundua kila kitu. Inawezekana ukawa unajiona unajua kila kitu kumbe kuna jicho la mama. Akiangalia kitu au mtu anapata jibu sahihi kuliko wewe," alisema siku ya Alhamisi.

Mwimbaji huyo mahiri aliwasihi watu kutilia maanani pingamizi zinazowekwa na wazazi wao bila kujali jinsi zinavyochukiza.

Pia aliwataka watu kuwasikiliza wazazi wa wenzao hasa kuhusu masuala ya uhusiano bila kujali jinsi mahaba yalivyo mazito.

"Unaweza kuona kama kwamba huyu mama hanipendi akiwa mama wa mwenzio kumbe  huenda anajua kwamba mtoto wake hayupo tayari ila anakosa au anashindwa jinsi ya kukufanya uelewe maana upo kwenye dimbwi la mapenzi," alisema.

"Akiwa mzazi wako ni rahisi kukukataza hata kwa kutumia nguvu zote ila ukiwa umezama humuelewi," 

Wakati huo, alifichua kwamba hapo awali karibu aingie kwenye ndoa mbaya ambayo mzazi wake alikuwa amemuonya dhidi yake.

"Mtu anayeitwa mzazi msikilize hata asiyekuwa wako," alisema.