Alikiba ajawa bashasha baada ya Joho kumuonyesha upendo mkubwa

Joho anajulikana kuupenda muziki wa Alikiba na urafiki wao umewapendeza wengi.

Muhtasari

•Joho ambaye ni rafiki wa karibu wa Alikiba alitumia akaunti yake ya Tiktok kuutangaza wimbo wake mpya 'Mahaba'.

•Alikiba ambaye alionekana kufurahishwa sana na video hiyo aliitaja kuwa ni remix ya Joho ya wimbo wa 'Mahaba'.

Alikiba na Joho
Image: HISANI

Staa wa Bongofleva Ali Saleh Kiba almaarufu Alikiba amejawa na bashasha baada ya aliyekuwa gavana wa kaunti ya Mombasa, Ali Hassan Joho kumuonyesha upendo mkubwa kwa kusapoti kibao chake kipya 'Mahaba'.

Joho ambaye ni rafiki wa karibu wa Alikiba alitumia akaunti yake ya Tiktok kuutangaza wimbo huo wake mpya kwenye jukwaa hilo kwa kufanya challenge ambayo imekuwa ikiendelea tangu kuachiwa wiki iliyopita.

Mwanasiasa huyo alijirekodi akiimba kipande kinachosema,  "Siku hizi hakuna mahaba. Mapenzi ya mkataba. Mpaka kufa yamekwisha."

Alikiba ambaye alionekana kufurahishwa sana na video hiyo aliitaja kuwa ni remix ya Joho ya wimbo wa 'Mahaba'.

Joho na mwanamuziki huyo mkongwe wana uhusiano wa karibu sana ambao wameonyesha hadharani mara nyingi.

Naibu kiongozi huyo wa ODM anajulikana kwa kuupenda muziki wa Alikiba na kwa urafiki wao unaowapendeza wengi.

Katika mahojiano ya hapo awali, Alikiba aliweka wazi kuwa bali na urafiki, amejifunza mengi kutoka kwa gavana huyo wa zamani.

"Ni rafiki yangu, kaka yangu mkubwa. Nimejifunza mengi kutoka kwake. Anapenda kutangamana na watu werevu,"  Alikiba alisema.

Bosi huyo wa Kings Music pia alisifia mafanikio makubwa ya mwanasiasa huyo na kukiri jinsi alivyochochewa naye.

"Ni mjasiri sana na anajua anachotaka kufanya. Nimejifunza mengi kutoka kwake ndiyo maana niko naye karibu," alisema.

Alikiba pia aliweka wazi kuwa gavana huyo wa zamani alikuwa akichangia sana katika maisha ya familia yake.

"Joho amekuwa kama baba mkubwa kwa watoto wangu. Amenitia moyo katika mambo mengi niliyofanya. Na nyie mnaweza kukubaliana nami na kujua kuwa Joho ni mzalendo wa hali ya juu na anajivunia kuwaongoza Wakenya, sio tu mashtaka yake katika kaunti ya Mombasa kama gavana," alisema 2021.

Mwanamuziki huyo alikuwa kwenye ndoa na Bi Amina Khalef kutoka Mombasa ila walitengana na kutalikiana mapema mwaka jana. Licha ya ndoa kuvunjika, wanandoa hao wa zamani wana watoto wawili pamoja.