Kwisha kabisa! Harmonize afuta tattoo ya Kajala na bintiye Paula huku akifurahia ukapera

Tattoo hiyo ambayo ameibeba kwa karibu mwaka mmoja imefunikwa.

Muhtasari

• Harmonize amefuta tattoo ya aliyekuwa mpenzi wake, Kajala Masanja na bintiye Paula ambayo alichorwa kwenye mguu wake mwaka jana.

•Mapema mwezi huu wakati alipofanya ziara ya muziki nchini Kenya, Harmonize alijibu kwa nini bado hakuwa ameifuta.

Harmonize na mchumba wake Kajala Masanja
Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Staa wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize hatimaye amefuta tattoo ya aliyekuwa mpenzi wake, Frida Kajala Masanja na binti yake Paula Paul ambayo alichorwa kwenye mguu wake mwaka jana.

Katika video yake akiimba na kucheza wimbo wake mpya, ‘Single Again’ aliyochapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram ilifichua kuwa tattoo hiyo ambayo ameibeba kwa karibu mwaka mmoja imefunikwa.

Mwimbaji huyo hata hivyo hajatoa maelezo kuhusu sababu yake ama wakati ambao alichukua hatua hiyo kubwa.

"Sijawahi kupenda wimbo wangu wowote kama ninavyoupenda wimbo huu," aliandika chini ya video hiyo.

Mwaka jana, wakati akiomba msamaha na kumsihi Kajala amrudie, Harmonize alipiga hatua ya kuchorwa tattoo ya picha ya kumbukumbu ya muigizaji huyo akiwa na bintiye Paula kwenye mguu wake. Alichukua hatua hiyo kama mojawapo ya njia ya kumtongoza ili warudiane baada ya kuwa wamekosana kwa mwaka.

Licha ya mahusiano yao kugonga ukuta mapema mwezi Desemba, mwimbaji huyo aliendelea kubeba tattoo hiyo kwenye mguu wake kwa zaidi ya miezi miwili kabla ya hatimaye kuchukua hatua ya kuifuta.

Mapema mwezi huu wakati alipofanya ziara ya muziki nchini Kenya, Harmonize alijibu kwa nini bado hakuwa ameifuta.

"Tatoo ni suala la kibinafsi. Sidhani kama ni kitu unaweza kuzungumza kuhusu.Tuangalie tu kama itakuwepo," alisema.

Wakati wa mahusiano yao, Harmonize na Kajala pia walichorwa tattoo za herufi ya kwanza ya majina yao kwenye vidole. Bado haijabainika wazi kama kwamba amefuta tattoo hiyo nyingine pia.

Wiki iliyopita, bosi huyo wa Kondegang alidokeza kwamba mara yake ya mwisho kufurahia tendo la ndoa ni wakati alipokuwa kwenye mahusiano na Kajala.

Akizungumza kupitia ukurasa wake wa Instagram, Konde Boy aliweka wazi kuwa hajashiriki mapenzi kwa miezi mitatu sasa.

Hata hivyo, hajaonyesha majuto yoyote ya kuwa bila mpenzi sasa kwani anadai hilo limemfanya kuwa na nguvu zaidi.

"Maisha ya kuwa single yanakufanya kuwa na nguvu.Miezi mitatu sijawahi kushiriki mapenzi. Najua hamuwezi kuamini hili," alisema kwenye video yake akimuinua mwanamke asiyejulikana na kufanya naye mazoezi.

Kwa kipindi cha takriban mwezi mmoja ambao umepita, bosi huyo wa Kondegang amekuwa akiweka wazi kwamba hayupo kwenye mahusiano yoyote na kuonyesha waziwazi jinsi anavyofurahia maisha ya kuwa single.

Mapema mwezi huu alisema kwa sasa anajipatia muda usiojulikana wa mapumziko kabla ya kujitosa kwenye mahusiano mapya.

"Msijali, hivi karibuni nitapata mtu na mtamjua!!," alisema.

Staa huyo wa Bongo alidokeza kwamba alipitia masaibu mengi mno wakati akiwa katika mahusiano yake ya awali.