Karen Nyamu ajibu kwa hasira baada ya kuulizwa ikiwa alimwacha Samidoh akiwaangalia watoto

"Aangalie watoto alafu wewe ukaimbe ama?" aljibu seneta huyo.

Muhtasari

•Shabiki aligundua kuwa Samidoh hakuwa kwenye picha na hivyo akamuuliza ikiwa alimwacha akiwachunga watoto.

•Takriban wiki mbili zilizopita, Nyamu na  Samidoh walionekana pamoja kwenye hafla ya mazishi ya shemeji wa naibu rais Rigathi Gachagua.

Karen Nyamu na Samidoh
Image: INSTAGRAM//

Wakili maarufu na seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu alikuwa mwanamke mwenye ghadhabu tele baada ya shabiki  kumuuliza kuhusu aliko baba ya watoto wake wawili wadogo, mwimbaji Samuel Muchoki almaarufu Samidoh.

Nyamu alikuwa amechapisha picha yake akiwa kwenye kikao cha hadhara siku ya Jumatatu na kuambatanisha na ujumbe wa motisha.

"SAFARI YAKO HAITAKUWA SAWA NA MTU MWINGINE YEYOTE. KWA HIVYO USIKUBALI DUNIA IKUAMBIE JINSI INAVYOPASWA KUONEKANA. HAKUNA MTU ALIYEWAHI KUPIGA HATUA KWA KUWA KAMA WOTE!," aliandika chini ya picha hiyo ambayo alichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Ingawa wanamitandao kadhaa walikubaliana na ujumbe huo na kuuthamini, kama ilivyo ada, kulikuwa na baadhi ya maoni yaliyoandikwa na wengine wao ambayo mama huyo wa watoto watatu hakuyapenda.

Shabiki mmoja aligundua kuwa Samidoh hakuwa kwenye picha na hivyo akamuuliza ikiwa alimwacha akiwachunga watoto.

"Hukuenda na kipochi chako ama ana baby seat 😂😂😂😂😂," mtumizi wa Instagram alimuuliza Bi Nyamu.

Mwanasiasa huyo ambaye alionekana kutopendezwa na ujumbe wa shabiki huyo alijibu, "Ababy seat alafu wewe ukaimbe ama?

Kumaanisha: (Aangalie mtoto alafu wewe ukaimbe ama)

Takriban wiki mbili zilizopita, Karen Nyamu na  Samidoh walionekana pamoja kwenye hafla ya mazishi ya shemeji wa naibu rais Rigathi Gachagua, Nancy Muthoni katika eneo la Gatanga, kaunti ya Murang'a.

Baada ya mazishi, Bi Nyamu alichapisha picha kadhaa za hafla hiyo  kwenye kurasa zake mbalimbali za mitandao ya kijamii.

Kati ya picha alizochapisha ni pamoja na moja ya mzazi mwenzake Samidoh akitoa hotuba yake kwenye hafla hiyo na nyingine inayoonyesha wakiwa wamekaa karibu na kuonekana kufurahia muda pamoja.

Siku moja baadaye, mkewe Samidoh, Edday Nderitu alimpa onyo mwimbaji huyo akimjulisha kuwa hayuko tayari kulea watoto wao katika ndoa ya wake wengi.

Kupitia taarifa ya uchungu kwenye ukurasa wake wa Facebook, mama huyo wa watoto watatu alimkashifu seneta huyo wa kuteuliwa akimtaja kama mtu asiye na maadili na asiyeheshimu familia yake.

"Nimemuomba Mungu kila siku anipe nguvu ya kukuombea lakini leo sina la kumwambia Mungu juu yako, umeniburuta na kuniweka mimi na watoto wangu kwenye bahari ya uchungu upate kukumbuka hili," Edday alimwandikia Samidoh.

Edday alidai kuwa mzazi mwenza wa mumewe, Karen Nyamu, anamzidi umri kwa miaka kumi, sababu nyingine ya kufanya akatae awe mke mwenzake.

Alibainisha kuwa ndoa yake ilikuwa nzuri siku za awali kabla ya mtu wa tatu kuingia ndani yake takriban miaka mitatu iliyopita.

"Imekuwa miaka 15 kamili ya ndoa iliyojaa panda shuka, ilikuwa mwanzo mdogo ambapo kidogo ilikuwa ya kutosha kwetu, kwa miaka mitatu iliyopita imekuwa maumivu,"