Kajala Masanja hatimaye afunguka ukweli kuhusu binti yake Paula kuolewa

Kajala ameweka wazi kuwa binti yake, Paula Paul bado hajaolewa.

Muhtasari

•Mpenzi huyo wa zamani wa Harmonize alibainisha kuwa binti yake Paula ni mdogo sana kuwa mke wa mtu.

•Paula na mama yake walizua gumzo kubwa mitandaoni baada ya kutangaza kwamba amejitosa kwenye ndoa.

Image: INSTAGRAM// PAUL KAJALA

Muigizaji mkongwe wa Filamu Bongo, Frida Kajala Masanja ameweka wazi kuwa binti yake, Paula Paul Kajala bado hajaolewa.

Huku akijibu maswali ya mashabiki wake nchini Burundi ambako yuko kwenye ziara ya kikazi ya siku chache, mpenzi huyo wa zamani wa bosi wa Kondegang, Harmonize alibainisha kuwa Paula ni mdogo sana kuwa mke wa mtu.

Kajala alifichua kuwa picha za hivi majuzi za bintiye akiwa amevalia gauni lililodaiwa kuwa la harusi ni tangazo tu ambalo lilifanikiwa.

"Nadhani Paula bado ni mdogo sana. Tulikuwa tunafanya tangazo na tumefanikiwa. Namaanisha, ndio. Watu walidhani kwamba ameolewa, Paula bado ni mdogo sana," alisema mama huyo wa binti mmoja.

Wiki jana, Paula na mama yake walizua gumzo kubwa mitandaoni baada ya kutangaza kwamba amejitosa kwenye ndoa.

Mwanamitindo huyo mwenye umri wa miaka 20 alichapisha picha kadhaa zilizoonyesha akiwa amevalia gauni maridadi la buluu huku akivishwa pete na kunyweshwa maziwa na mwanaume ambaye sura yake ilifichwa.

"Asante mume Wangu❤️💍," aliandika chini ya picha hiyo.

Kajala alimpongeza binti huyo wake wa pekee na kumtakia heri njema katika maisha yake mapya ya ndoa.

"Mungu akutangulie katika maisha yako haya mapya dada pau ukawe mke bora sio bora mke, Bi Ally," aliandika kwenye Instagram.

Wengi hata hivyo tayari walikuwa wameshuku kuwa yote ilikuwa kiki na mpenzi huyo wa zamani wa Rayvanny bado hajaolewa.

"Acheni uongo wasanii jamani," binamu ya Diamond Platnumz, Rommy Jons alijibu chini ya chapisho la Kajala.

Wiki chache zilizopita, bosi wa Next Level Music, Rayvanny alidokeza kuwa bado angali na hisia za mapenzi kwake.

Msanii huyo wa zamani wa WCB alichapisha picha ya binti huyo wa pekee wa Kajala Masanja na chini yake kuambatanisha na emoji za moyo wenye moto, ambazo kwa kawaida hutumika kuashiria mapenzi.

"❤️‍🔥❤️‍🔥❤️‍🔥❤️‍🔥,"  aliandika kwenye picha nzuri ya kipusa huyo mwenye umri wa miaka 20 ambayo alipakia Instagram.

Hatua hiyo ilidokeza kuwa huenda wawili hao bado wana uhusiano mzuri licha ya kudaiwa kuachana zaidi ya mwaka mmoja uliopita. Baadhi walichukulia kitendo cha Rayvanny kama dokezo kuwa wamerudiana.