"Sikuwa mke, nilikuwa mtumwa!" Amira afunguka masaibu ya ndoa yake na Jamal Rohosafi

Amira amemtaka Jamal ampe talaka zote tatu akidai kuwa alimpa talaka moja pekee.

Muhtasari

•Amira alidai kuwa baba huyo wa watoto wawili alimnyanyasa kwa takriban miaka miwili kabla ya kugura ndoa hiyo.

•Alibainisha kuwa sasa yuko huru kabisa na akamfahamisha mumewe huyo wa zamani kuwa hawezi tena kumtawala.

Amira na Jamal Rohosafi
Image: INSTAGRAM//

Siku ya Ijumaa asubuhi, aliyekuwa mke wa mfanyabiashara mashuhuri Jamal Rohosafi, Amira alifanya kipindi cha moja kwa moja kwenye mtandao wa Instagram ambapo alifunguka kuhusu masaibu ya ndoa yao ya muda mrefu.

Katika kipindi hicho, alidai kuwa baba huyo wa watoto wawili alimnyanyasa kwa takriban miaka miwili kabla ya kugura ndoa hiyo.

Amira alifananisha ndoa yake na utumwa akidai hakuwa na uhuru kwani mfanyibiashara huyo alimtawala kwa karibu kila kitu.

"Jamal huwezi kunitawala tena. Ulikuwa unanitawala, ulikuwa unanidanganya. Hata sikuwa mke, nilikuwa mtumwa katika nyumba hiyo.

Hakuna siku ulinipa heshima. Hakuna siku uliniheshimu kama mke wako. Ulinifanya nijichukie. Nilijipoteza," alisema kwa uchungu mwingi.

Mama huyo wa wavulana wawili alidai kuwa Jamal alikuwa akimtishia kiasi kwamba hangeweza kufunguka kuhusu masaibu yake.

Hata hivyo alibainisha kuwa sasa yuko huru kabisa na akamfahamisha mumewe huyo wa zamani kuwa hawezi tena kumtawala.

"Sasa hivi mimi si kijakazi. Mimi si mtu niliyekuwa kwa miaka mitano. Huwezi kunizuia kuzungumza sasa hivi," alisema.

Kufuatia hayo, Amira aliweka wazi kwamba sasa tayari amemaliza uhusiano wake na baba huyo wa watoto wake wawili na kumtaka ampe talaka zote tatu akidai kuwa alimpa talaka moja pekee.

"Jamal niandikie talaka zangu tatu. Uliniandikia moja tu. Nataka zikiwa tatu kwa sababu nimemaliza. Nimemalizana na wewe kabisa," alisema.

Kwenye mahojiano na Eve Mungai, Jamal alitupilia mbali madai kwamba aliachwa na mama huyo wa watoto wake.

Alidai kwamba yeye ndiye aliyemuacha mfanyibiashara huyo wa vipodozi na kueleza kuwa baada ya kumuacha, Amira alifanya jitihada za kujaribu kurudi nyumbani kwake mara mbili lakini akawa anazuiliwa, na kuwa hilo ndilo jambo linalompa hasira za kumzungumzia kwa mabaya mitandaoni.

“Ni mimi ndio nilimuandikia na nikasema asiwahi kanyaga kwa nyumba yangu. Mimi ndio nilimuacha na si yeye aliniacha kama anavyowadanganya kwa mitandao ya kijamii. Na kama yeye ndio angekuwa ananiacha hangekuwa anateta eti kwa nini sijampa hivi vitu vya nyumba? Mbona amenifuata kwa nyumba yangu mara mbili akafukuzwa? Ni kitu cha kutumia akili, kwa hiyo aache kudanganya watu huko nje…alisema.

Wawili hao wamekuwa wakitupiana cheche za maneno na kuchafuana kwenye mitandao siku za hivi majuzi.