"Sina uwezo, huyu mmoja ni mzigo!" Guardian Angel afunguka kuhusu kuoa mke wa pili

Guardian Angel alikiri inaweza kuwa vigumu kwake kuwezana na wanawake wawili kwani Musila pekee humchokesha wakati mwingine.

Muhtasari

•Akizungumza na waandishi wa habari, Guardian Angel aliweka wazi kuwa ameridhika sana na mke wake mmoja, Bi Esther Musila.

•Angel alibainisha kuwa baadhi ya wanafamilia wake walikuwa na wake zaidi ya mmoja lakini haikuishia vyema kwao.

Image: INSTAGRAM// GUARDIAN ANGEL

Mwimbaji wa nyimbo za injili Peter Omwaka almaarufu Guardian Angel amefutilia mbali uwezekano wa yeye kuoa mke wa pili.

Akizungumza na waandishi wa habari, Guardian Angel aliweka wazi kuwa ameridhika sana na mke wake mmoja, Bi Esther Musila.

Mwanamuziki huyo mahiri mwenye umri wa miaka 33 alikiri kwamba inaweza kuwa vigumu sana kwake kuwezana na wanawake wawili kwani Bi Musila pekee yake humchokesha wakati mwingine.

"Neema yangu hainiruhusu, sina huo uwezo. Hata huyu mmoja saa zingine ni mzigo kidogo. Mwanamke mmoja tu pia sio mchezo. Majukumu ya huyu mmoja sio mchezo," alisema.

Guardian Angel alibainisha kuwa baadhi ya watangulizi wake katika familia yao walikuwa na wake zaidi ya mmoja lakini haikuishia vyema kwao.

"Siwezi taka kujiingisha kwa shimo kama hilo. Mwanaume unaweza kuwa mtulivu zaidi na kukua zaidi ukiwa na mke moja tu," alisema.

Mwimbaji huyo wa nyimbo za injili alikiri kuwa mara nyingi hupokea jumbe za mapenzi kwenye kurasa zake mbalimbali za mitandao ya kijamii kutoka kwa wanawake wakikiri kumpenda. Hata hivyo alisema kuwa kwa kawaida huwapuuza au hata kuwablock watumaji kwani yuko kwenye ndoa yenye furaha na Musila.

"Mimi nawaruhusu kunipenda. Lakini ikifika kwa upendo wa kindoa, tayari nina pete. Si kwa sababu ya pete tu, niko na mtu ninayependa  kindoa. Ile upendo ingine ya kawaida naruhusu kabisa, lakini ya kindoa, niko hapa nafurahi," alisema.

Takriban mwezi mmoja uliopita, Guardian Angel aliweka wazi kwamba amepata mafanikio mengi katika miaka minne ambayo amekuwa kwenye mahusiano ya mapenzi na mke wake Esther Musila.

Akizungumza kwenye mahojiano ya YouTube na Willy M. Tuva , mwimbaji huyo alitaja uhusiano wake na mama huyo wa watoto watatu wakubwa mwenye umri wa miaka 53 kuwa muunganisho sahihi.

“Yamebadilisha maisha yangu, ukimsikiliza akiongea (Bi Musila) atasema jinsi mahusiano yetu yamebadilisha maisha yake,” alisema.

Angel alidokeza kuwa athari chanya ya mahusiano yao ndilo jambo muhimu zaidi bila kujali maneno hasi kutoka ya wakosoaji .

Aidha, alifichua kwamba ameweza kukua katika nyanja nyingi za maisha tangu alipojuana na mwenzi huyo wake wa maisha.

“Nimeweza kuwa na ufanisi, nimeweza kukua, sio tu kimwili, lakini nimeweza kukua hata kiuchumi. Hata vitu kama hii ukulima yangu, na sifanyi ukulima kwa shamba ya watu, nafanya kwangu. Hiyo yote imeweza kufanyika kwa sababu ya muungano ambao niko nao na mke wangu," alisema Guardian Angel.

Mwanamuziki huyo alikashifu wote wanaopinga ndoa yake akisema kuwa wao ni watu wenye wivu na wapuuzi. Kufuatia hilo, aliwataka kuzingatia kuboresha maisha yao na kuacha kujiingiza katika biashara za watu wengine.

Guardian hata hivyo alikiri kuwa matusi mengi ambayo huelekezwa kwa mkewe kwa kawaida hufanya ahisi vibaya.

"Naskia vibaya sana. Kwa kweli najisikia kuchukizwa sana na kuguswa sana kwa sababu huyu ni mtu ninayempenda sana. Sisi sote tunaweza kuona hilo," alisema.

Alisema kwamba ndoa yake imekuwa mzuri huku akibainisha kuwa kuna wanaume wengi ambao wameoa wanawake wadogo kiumri lakini wanaishia kutengana.