“Hakuna mbegu ya kiume yenye nguvu kufikia mayai yangu!” Huddah akana ujauzito

Mwanasoshalaiti huyo alikuwa ametangaza kuwa ana ujauzito wa miezi mitatu.

Muhtasari

•Katika taarifa yake fupi siku ya Jumatatu, mfanyibiashara huyo wa vipondozi alifichua kwamba ana ujauzito wa miezi mitatu.

Image: INSTAGRAM// HUDDAH MONROE

Mwanasoshalaiti mashuhuri wa Kenya, Alhuda Njoroge ametupilia mbali madai yake ya awali kwamba ni mjamzito.

Katika taarifa yake fupi siku ya Jumatatu, mfanyibiashara huyo wa vipondozi alidai kwamba ana ujauzito wa miezi mitatu.

"Ujauzito wa miezi mitatu," aliandika kwenye Instagram.

Aliambatanisha ujumbe wake na video yake akinengua kiuno ndani ya eneo moja la burudani jijini Nairobi. Kwenye video, alijifunga leso kiunoni na kuvalia sidiria pekee upande wa juu hivyo kuacha tumbo lake lililochomoza kidogo kuonekana.

Huddah alionekana mchangamfu na mwenye nguvu alipokuwa akidensi na wengine waliokuwa wamejumuika kwenye klabu hiyo.

Siku moja baadaye hata hivyo, alijitokeza tena kupinga madai yake ya awali kuwa anatarajia mtoto wake wa kwanza.

"Nyie, mimi sio mjamzito," alisema.

Mwanasoshalaiti huyo alieleza kwamba tumbo lake limeendelea kuwa kubwa na hivyo kufanya aonekane mjamzito.

Wakati huohuo, alidokeza kuwa hana mpango wa kupata mtoto hivi karibuni.

"Niko kwenye awamu yangu ya kuwa mwanamke mzima, tulieni. Hakuna mbegu ya kiume yenye nguvu ya kutosha kushika mayai yangu," alisema.

Kwa muda mrefu, mwanasoshalaiti huyo mzaliwa wa Nairobi amekuwa akiweka mahusiano yake kuwa siri. Ni mara chache tu ambapo ameonekana akizungumza kuhusu mpenzi wake lakini mara kadhaa ameonyesha kumpenda sana mwanamume huyo ambaye bado hajajulikana hadharani.

Mwaka jana, alidaiwa kutoka kimapenzi na mwimbaji wa Tanzania Juma Jux baada ya wawili hao kuonekana wakiwa pamoja mara kadhaa.

Wawili hao hata hivyo walijitokeza kuweka wazi kuwa hakuna mahaba kati yao na kudai kwamba uhusiano wao ni wa kirafiki na kibiashara tu.