Akothee afichua kikosi cha wapambe atakachopeleka Uswizi kwa harusi yake ya pili

Alibainisha anaolewa mwaka mzima wa 2023 na kuwataka wengine kupanga harusi zao mwaka ujao.

Muhtasari

•Akothee alifichua majina 17 ya watu ambao watapamba hafla hiyo ya pili wakiwemo mabinti zake; Vesha, Rue Baby na Fancy Makadia.

•Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 53 amewashukuru 17 hao kwa kupamba harusi ya Aprili 10.

•Akothee alibainisha anaolewa mwaka mzima wa 2023 na kuwataka watu wengine kupanga harusi zao mwaka ujao.

wakicheza na wapambe wa harusi yao mnamo Aprili 10, 2023.
Akothee na mumewe Denis Shweizer wakicheza na wapambe wa harusi yao mnamo Aprili 10, 2023.
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mke mpya zaidi mjini, Esther Akoth almaarufu Akothee ametangaza kuwa atapeleka kikosi chake kizima cha wapambe wa harusi hadi nchini Uswizi kwa sehemu ya pili ya harusi yake itakayofanyika Julai 10, 2023.

Siku ya Alhamisi, mama huyo wa watoto watano alifichua majina 17 ya watu ambao watapamba hafla hiyo ya pili wakiwemo mabinti zake watatu; Vesha Okello, Rue Baby na Fancy Makadia. Wengine ni pamoja na mbunge  wa Lang'ata Jalang'o, Kabi na Milly Wajesus, Azziad Nasenya,  Mimi, Janet Otieno, Nina Ajigo, Fiona Morema, Lulu, Mokeira Onchiri, Evander Holyfield, Beatrice Schnelli Okello na Geret.

Kabla ya siku hiyo kubwa,  mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 53 amewashukuru 17 hao kwa kupamba harusi ya Aprili 10.

"Ninawathamini sana. Asanteni sana kwa upendo. Sapoti ya ajabu. Nawapenda," aliwaandikia kwenye mtandao wa Instagram.

Mama huyo wa watoto watano alibainisha anaolewa mwaka mzima wa 2023 na kuwataka watu wengine kupanga harusi zao mwaka ujao.

Akothee na mume wake Denis Schweizer almaarufu Omosh walifunga pingu za maisha siku ya Jumatatu, Aprili 10, katika hafla ya harusi ya kupendeza iliyofanyika katika Windsor Golf Hotel & Country Club, jijini Nairobi, Kenya.

Kabla ya hafla hiyo, mwanamuziki huyo alikuwa amedokeza kwamba kutakuwa na sehemu ya pili ya harusi itakayofanyika Uswizi.

Akizungumza na waandishi wa habari wiki jana baada ya kumlaki nchini bintiye Fancy Makadia,  Akothee aliweka wazi kuwa ni wanawe wawili wanaoishi Ufaransa, Prince Ojwang na Prince Oyoo hawangeweza kufika kwenye harusi yake ya Aprili 10 kwa sababu ya sheria za shule yao lakini akadokeza kwamba wawili hao watashuhudia sherehe ya pili iliyoratibiwa kufanyika Uswizi mnamo Julai 10.

"Karibu Prudence Vanpelt, bintiye Akothee. Msilete propaganda na siasa za familia kwa harusi yangu. Watu pekee ambao watakosa harusi yangu ni wanangu wawili ambao hawatafanikiwa kwa sababu ya sheria za shule, lakini watashuhudia ambayo imeratibiwa kufanyika Julai 10. Mwaka mzima Akothee anaolewa," alisema.

Harusi ya Akothee na Shweizer ni yake ya pili kwani alifunga ndoa kwa mara ya kwanza na baba ya binti zake watatu, Jared Okello zaidi ya mwongo mmoja uliopita. Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 hapo awali aliwahi kufichua kuwa harusi yake na Bw Jared iligharimu shilingi  2,500 pekee.