"Nimeitwa, naanza kuimba injili" Akothee atangaza baada ya Pastor Ezekiel kutambua ndoa yake

Akothee amesherehekea kwamba hatimaye amefikiwa na mtumishi huyo wa Mungu.

Muhtasari

•Ezekiel alitumia mfano wa Akothee kuwatia moyo akina mama wasio na waume kuwa pia wao watapata wachumba wa kufunga  ndoa nao hivi karibuni.

•Akijibu mahubiri ya Bw Ezekiel, mama huyo wa watoto watano, kwa mzaha alidokeza kuwa ataanza kuimba nyimbo za injili.

Akothee, Denis Shweizer, Pastor Ezekiel
Image: HISANI

Mwimbaji Esther Akoth almaaruf Akothee amejawa na bashasha baada ya mchungaji Ezekiel Odero kutambua hatua yake kuolewa.

Bw Ezekiel wakati wa ibada ya krusedi iliyofanyika katika mtaa wa Bombolulu, Mombasa wiki iliyopita alihubiri kuhusu mambo mengi ikiwa ni pamoja na mahusiano na ndoa. Pia aliwaombea wenye matatizo mbalimbali ya maisha.

Mtumishi huyo wa Mungu aliwaombea waumini wa kike wasio na waume wapate kuolewa huku akikemea nguvu za giza zinazowazuia kupata waume. Ni wakati huo ambapo alitumia mfano wa Akothee kuwatia moyo akina mama wasio na waume kuwa pia wao watapata wachumba wa kufunga  ndoa nao hivi karibuni.

"Kama ata yule binti anaitwa Akothee, aliyekuwa akiitwa rais wa kina mama single ameolewa, wewe pia uolewe kwa jina la Yesu Kristo," mchungaji huyo aliwaambia waumini waliokuwa wamejumuika kwenye mkutano huo.

Aliongeza, "Kama rais ameolewa, mawaziri, na CAS pamoja na wafanyikazi wote  wa serikali, wote waolewe."

Mtumishi huyo wa Mungu alikiri kwamba alifurahi sana kumona mwimbaji huyo wa miaka 43 akiolewa. Alisema ilimpa matumaini kwamba akina mama wengine wasio na waume watapata wenzi wa ndoa.

"Niliona nikafurahi. Nikasema ikiwa rais wa single mothers ameolewa, kina mama wote single wapate roho ya ndoa," alisema.

Akothee sasa amesherehekea kwamba hatimaye amefikiwa na mtumishi huyo wa Mungu.

Akijibu mahubiri ya Bw Ezekiel, mama huyo wa watoto watano, kwa mzaha alidokeza kuwa ataanza kuimba nyimbo za injili.

"Aah Pastor Ezekiel amenifikia. Akothee mkubwa, Sasa nimeitwa, Ninaruka kutoka kwa muziki wa kidunia hadi kwenye Injili, nani anabishaa," alisema.

Akothee na mchumba wake Dennis Shweizer almaarufu Mister Omosh walifunga pingu za maisha katika harusi ya kifahari iliyofanyika Windsor Golf Hotel & Country Club, jijini Nairobi mnamo Aprili 10.

Harusi ya mama huyo wa watoto watano ilipambwa na wanafamilia, marafiki wa karibu, wasanii na wanasiasa mashuhuri nchini. Jumla ya watu wasiopungua 300 walikuwa wamealikwa katika hafla hiyo ya kukata na shoka. Ilikuwa ni harusi ya Akothee  ya pili kwani alifunga ndoa kwa mara ya kwanza na baba ya binti zake watatu, Jared Okello zaidi ya mwongo mmoja uliopita.