Kajala amtupia vijembe Harmonize baada ya kumtambulisha mpenziwe mpya

Muigizaji huyo alibainisha kuwa Mungu aliwaondoa 'baadhi ya watu' katika maisha yake kwa makusudi,

Muhtasari

•Kajala ameonekana kumtupia vijembe aliyekuwa mpenzi wake, Harmonize siku moja tu baada ya kumtambulisha mpenzi wake mpya.

•Harmonize alibainisha kuwa mpenzi wake mpya ni zaidi ya wanawake wote ambao aliwahi kuchumbiana nao.

Kajala, Harmonize, Phiona
Image: HISANI

Muigizaji wa filamu Bongo, Frida Kajala Masanja ameonekana kumtupia vijembe kwa njia isiyo ya moja kwa moja aliyekuwa mpenzi wake, mwanamuziki Harmonize siku moja tu baada ya kumtambulisha mpenzi wake mpya.

Siku ya Jumatatu, Konde Boy ambaye amekuwa akiishi maisha ya ukapera kwa miezi mitano alifichua kuwa amezama kabisa kwenye dimbwi la mahaba na mwanasosholaiti wa Rwanda Phiona almaarufu Yolo the Queen.

Jumanne, Kajala Masanja alitumia meme kuashiria kwamba Mungu aliwaondoa 'baadhi ya watu'  katika maisha yake kwa makusudi, akionekana kumzungumzia mwimbaji huyo aliyechumbiana naye kwa miezi kadhaa.

"Mungu huondoa watu kutoka kwa maisha yako kwa sababu alisikia mazungumzo ambayo hukusikia," alishiriki kwenye Instagram.

Muigizaji huyo alitangaza mwisho wa mahusiano yake na Harmonize mwishoni mwa mwaka jana baada ya kuchumbiana naye kwa takriban miezi saba. Wawili hao walikuwa wamerudiana Mei baada ya kutengana mwaka wa 2021.

Wakati akitangaza kuachana na bosi huyo wa Konde Music Worldwide mwezi Desemba, Kajala aliweka wazi kwamba alikuwa tayari kupiga hatua nyingine baada ya mahusiano yao ya miezi michache kugonga mwamba.

Ingawa hakufichua kilichowatenganisha, aliweka wazi kwamba hakubeba kinyongo chochote dhidi ya mwimbaji huyo.

"Mimi kama mwanamke na binadamu nimeumbwa kupenda na kusamehe pia, ila kwenye hili nastahili kuchekwa, nastahili kubezwa na kudharauliwa pia. Sipo hapa kujitetea wala kutia huruma ni kweli nilifanya makosa na nimeyagundua makosa yangu, mimi siyo mkamilifu," Kajala alisema wakat huo.

Image: INSTAGRAM// KAJALA MASANJA

Jumatatu, Konde Boy aliweka wazi kwamba hayuko single tena huku akimtambulisha Phiona kama mpenziwe mpya.

"Sawa, siko single tena nimechukuliwa tayari," mwimbaji huyo alisema kwenye ukurasa wake wa mtandao siku ya Jumatatu.

Harmonize alidokeza amemfahamu Phiona kwa miaka minne iliyopita akitaja kuwa ni wakati mwafaka wa kujaribu mahusiano.

Huku akionekana kuwatupia vijembe wapenzi wake wa zamani k.v Kajala Masanja, Wolper na Sarah Michelloti, alibainisha kuwa mwanasosholaiti huyo wa Rwanda ni zaidi ya wanawake wote ambao aliwahi kuchumbiana nao.

"Naona ni wakati wa kukuonyesha jinsi nilivyo mwanaume wa kweli. Nakupenda sana Yolo The Queen. Umepita kila msichana niliyekutana naye maishani mwangu. Umenifanya hata nijisikie kuwa mimi ni Mnyarwanda," alisema.

Aliendelea kudokeza kwamba hata anapanga kununua nyumba nchini Rwanda ili mradi tu kuwa karibu na mpenzi wake mpya.

Ili kuthibisha mapenzi yake kwa mlimbwende huyo, staa huyo wa bongo fleva alidokeza kwamba anapanga kuchorwa tattoo yake ambayo kulingana naye, itakuwa ya mwisho kabisa kuchorwa mwili mwake.

"Sawa, napata tattoo yangu ya mwisho. Sitokuja choraga tena. Bila shaka ni ya uso wako mzuri Phiona," alisema.