"Umeniweka line, ningekuwa sherehe" Diana amsifia Bahati kwa kumtoa kwenye maisha ya anasa

Alisema Bahati alimfanya atulie naaweze kupata mwelekeo wa maisha kiasi kwamba sasa anafurahia mafanikio makubwa.

Muhtasari

•Diana alibainisha kuwa ikiwa hangeolewa na Bahati angekuwa akirukaruka kutoka eneo moja la burudani hadi lingine ili kujivinjari na kuburudika.

•"Ona Mungu, nayo umenieka kwa line, nikakuwa na malengo maishani mpaka sasa mimi ni Aunty Madooo, wueeeh," Diana alisema.

Diana Marua na mumewe Bahati
Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA

Mwanavlogu Diana Marua amekiri kuwa mume wake Kelvin Kioko almaarufu Bahati alimsaidia kuyaaga maisha ya anasa na kutulia.

Siku ya Jumatano, mama huyo wa watoto watatu alibainisha kuwa ikiwa hangeolewa na Bahati zaidi ya nusu mwongo uliopita basi angekuwa akirukaruka kutoka eneo moja la burudani hadi lingine ili kujivinjari na kuburudika.

"Sasa kama hungenioa, leo ndio ningekuwa naanza sherehe halafu singeelewa vile Friday ningekuwa Naks, Sunday nijipate Narok, Monday ndio nishike bearing," alisema kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.

Rapa huyo mwenye umri wa miaka 34 alisema Bahati alimfanya atulie kabisa na aweze kupata mwelekeo wa maisha kiasi kwamba sasa anafurahia mafanikio makubwa. Alimshukuru sana kwa jambo hilo.

"Ona Mungu, nayo umenieka kwa line, nikakuwa na malengo maishani mpaka sasa mimi ni Aunty Madooo, wueeeh," alisema.

Mwezi uliopita, Diana alifichua hakuwa tayari kwa ndoa wakati alipokutana na mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili.

Akizungumza kwenye YouTube, mama huyo wa watoto watatu alidai kwamba Bahati alimnasa kwenye ndoa yao ya sasa.

Wanandoa hao walikuwa wanashiriki mazungumzo kuhusu maisha yao ya siku za nyuma wakati Diana Marua alipofichua kuwa Bahati alimpa ujauzito katika mwezi wa saba wa uchumba wao na kuwapelekea kwenye ndoa.

Ulininasa katika mwezi wa saba. Ulininasa. Lakini mpenzi ulikuwa unanipenda. Ulikuwa unakuja na hiyo Mercedes ya bluu kutoka Ruaka hadi Syokimau. Sijui mbona ulikuwa unakuja kwangu saa sita usiku," Diana alisimulia.

Kwenye mazungumzo hayo, Bahati alibainisha alimsaidia mwanavlogu huyo kuacha maisha ya anasa na kuanzisha familia.

"Kama isingekuwa mimi, zile klabu zinafungwa zingekuwa zinafungwa ukiwa ndani. Ungekuwa huko tu unaserereka unauliza utapata watoto lini alafu unajibu 'bado niko mdogo'" Bahati alimwambia mkewe.

Aliongeza,"Mimi ndio nilikwambia haya mambo ya kuwa mdogo."

Diana Marua kwa upande wake alimweleza mwanamuziki huyo kwamba hangekuwa katika nafasi ambayo yuko kwa sasa ikiwa hangekuja katika maisha yake zaidi ya nusu muongo uliopita.

"Naweza kukuambia kitu? Unajua isingekuwa mimi, leo usingekuwa na nyumba hii. Isingekuwa mimi, usingepata watoto hawa. Isingekuwa mimi, usingekuwa na magari manne yameegeshwa hapa," Diana alimkumbusha Bahati.

Mama huyo wa watoto watatu alimweleza mwimbaji huyo kwamba usaidizi ambao amempa ni dhibitisho la kweli la mapenzi.