Rais wa wasioamini uwepo wa Mungu ataka kuachiliwa kwa Yesu wa Tongaren mara moja!

Harrison Mumia alidai kwamba Yesu wa Kibiblia sio wa ukweli na kuitaka mahakama kama inaamini ni wa ukweli kumwasilisha mahakamani.

Muhtasari

• “Yesu wa Tongaren yupo, na kwa kadiri tunavyohusika, haongozi madhehebu. Polisi wana bidii kupita kiasi kwa kumkamata,” Bw Mumia alisema.

• Hakimu mfawidhi wa mahakama ya Bungoma Tom Mark Olando alitoa kibali kwa polisi kumshikilia Yesu kwa siku nne Zaidi ili kufanyiwa uchunguzi wa kiakili

Yesu wa Tongaren kufanyiwa uchunguzi wa akili.
Yesu wa Tongaren kufanyiwa uchunguzi wa akili.
Image: Maktaba

Kiongozi wa wasio amini katika uwepo wa Mungu nchini Kenya, Harrison Mumia ameitaka Huduma ya Kitaifa ya Polisi kumwachilia huru kiongozi wa Kanisa la New Jerusalem Church lenye makao yake mjini Bungoma Bw Eliud Wekesa almaarufu Yesu wa Tongaren mara moja pasi na shuruti yoyote.

Katika taarifa, Mumia kupitia chama chao cha wakana Mungu Kenya, walitoa changamoto kwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi kuwasilisha Yesu halisi mahakamani ikiwa wanataka kesi yao dhidi ya Yesu wa Tongaren isimamishwe.

"Tunadai kuachiliwa mara moja kwa Yesu wa Tongaren. Ni lazima polisi wamtoe Yesu halisi ikiwa dai lao ni kwamba mtu huyu si Yesu Kristo halisi, Mwana wa Yahwe!” AIK ilisema katika taarifa iliyotiwa saini na kiongozi wake Harrison Mumia.

Kulingana na Mumia, Yesu wa Kibiblia ni mhusika wa kubuniwa, aliyebuniwa na dini zinazodai kuwa za Kikristo, tofauti na Yesu wa Tongaren ambaye yuko katika maisha halisi.

“Yesu wa Tongaren yupo, na kwa kadiri tunavyohusika, haongozi madhehebu. Polisi wana bidii kupita kiasi kwa kumkamata,” Bw Mumia alisema.

Muungano huo tata ulitoa taarifa hiyo saa chache baada ya mahakama ya Bungoma kutoa kibali kwa wachunguzi kumshikilia Yesu wa Tongaren kwa siku nne Zaidi hadi Mei 16.

Hakimu mfawidhi wa mahakama ya Bungoma Tom Mark Olando alitoa kibali kwa polisi kumshikilia Yesu kwa siku nne Zaidi ili kufanyiwa uchunguzi wa kiakili kabla ya kupandishwa kizimbani tena Jumanne wiki kesho.

Upande wa mashtaka ulikuwa umeomba muda wa siku saba kwa uchunguzi kamili kuhusu mafundisho na shughuli za Wekesa.

Katika hati yake ya kiapo, upande wa mashtaka ulidai kanisa la Wekesa, New Jerusalem, halijasajiliwa kisheria.

Wekesa alijiwasilisha kwa polisi kwa hiari Jumatano kufuatia wito wa kuhojiwa kuhusu mafundisho na shughuli zake za kidini.