Video: Wahubiri wakabana koo katika soko la Gikomba wakigombania eneo la kuhubiri

Mchungaji wa kike alikuwa analia kwa sauti za kutisha kama anaomboleza baada ya mchungaji wa kiume kutwaa eneo lake la kuhubiri.

Muhtasari

• Mchungaji wa kike alipiga magoti na kuchomoa Biblia kutoka mkobani pake huku akizungusha kitambaa hewani akiendelea kuomboleza.

• Vituko hivyo vyote vilionekana kutomtisha mchungaji wa kiume ambaye alivitaja kama vya kishirikina.

Wahubiri wagombania eneo la kuhubiri sokoni Gikomba
Wahubiri wagombania eneo la kuhubiri sokoni Gikomba
Image: Screengrab//TikTok

Video ya wachungaji wawili, wa kike na wa kiume wote wakiwa na Biblia mikononi tayari kuwapakulia wafanyibiashara wa soko la Gikomba neno imeenea mitandaoni baada yao kuonekana wakigombana vikali.

Katika video hiyo ambayo ilipakiwa TikTok, wahubiri hao wawili walionekana wakimenyana vikali kwa maneno na kwa wakati mwingine kutishia kukabana, huku ikidaiwa kwamba walikuwa wanapigania eneo la kuhubiri kwenye kichochoro kimoja sokoni humo.

Mchungaji wa kiume alionekana akihubiri kwa kunukuu maneno kutoka kwa Biblia yake katika eneo hilo wakati yule wa kike ambaye alikuwa amevalia rinda la rangi nyekundu iliyoyeyuka akifika pale huku akitoa sauti kama ya kuomboleza baada ya eneo lake la mahubiri kutwaliwa na huyu wa kiume.

Hata hivyo, sauti za kutisha za yule mchungaji wa kike zilionekana kabia kutomtikiza mchungaji wa kiume ambaye aliendelea kuwapa watu waliojaa pale kwa mshangao neno, na kumtuhumu mchungaji huyo wa kike kwa kutoa mafunzo ya kupotosha kama yale ya mchungaji Paul Mackenzi kutoka Kilifi.

“Enda na huko, lia kabisa. Hamwezi kudanganya watu, Mackenzi alianikwa kwa kudanganya na kutaka kutoa kafara watu kule Shakahola, Ezekiel akaanikwa na wewe huwezi danganya watu hapa…” mchungaji huyo wa kiume alimsimangqa vikali yule wa kike.

Mchungaji mwanamke aliendelea na sarakasi zake ikiwemo kupiga magoti ardhini na kuingia kwenye mkoba wake ambapo alitoa Biblia yake na kuifungua huku akitoa kitambaa shingoni pia na kuanza kukizungusha hewani kama mpeperusha bendera.

Vituko hivyo vyote vilionekana kutomtisha mchungaji wa kiume ambaye alivitaja kama vya kishirikina huku akimpa nafasi ya kuendelea kuwaonesha watu sinema ya bila malipo.

Vilio na maombolezo ya mchungaji wa kike viliwavutia makumi ya wafanyibiashara ambao baadhi yao walionekana kumtetea kwa kumkanya mchungaji wa kiume dhidi ya maneno yake makali kwa mchungaji mwanamke kwa kulinganisha mahubiri yake na matukio ambayo yameteka nchi kwa Zaidi ya mwzi mmoja kutoka shamba la Shakahola.

Hii hapa ndio video ya tukio hilo la kusisimua: