Dadake Diamond ajawa bashasha baada ya 'Mmakonde' wake kuchorwa tattoo ya jina lake

Esma alidaiwa kuwa kwenye mahusiano na Harmonize kutokana na uhusiano mzuri ulioonekana baina yao.

Muhtasari

•Esma alionyesha kifua cha mwanaume ambaye kichwa chake kilifichwa akiwa na tattoo ya jina Esma na mchoro wa moyo chini yake.

•Hivi majuzi, dada huyo wa Diamond alidaiwa kuwa kwenye mahusiano na Harmonize kutokana na uhusiano mzuri ulioonekana baina yao.

Esma na kaka yake Diamond
Image: HISANI

Siku ya Jumanne, dada mkubwa wa Diamond Platnumz,  Esma Khan alimshukuru mpenzi wake asiyejulikana kwa kuchorwa jina lake kwenye kifua chake.

Kwenye Instagram, alionyesha kifua cha mwanaume ambaye kichwa chake kilifichwa akiwa na tattoo ya jina Esma na mchoro wa moyo chini yake.

Katika video aliyochapisha, alionekana akiwa ameshika shingo ya mwanaume huyo ambaye alijilaza kitandani bila shati.

"Ooh Mmakonde wangu jamani nakupenda nikupe zawadi gani mimi!??" alisema chini ya video ya mwanaume huyo ambayo alichapisha.

Chapisho hilo ni dokezo kwamba mama huyo wa watoto watatu amezama kabisa katika dimbwi la mahaba na mpenziwe asiyetambulishwa.

Hivi majuzi, dada huyo wa Diamond alidaiwa kuwa kwenye mahusiano na Harmonize kutokana na uhusiano mzuri ulioonekana baina yao.

Mwezi uliopita Konde Boy alibainisha kuwa dada huyo wa hasidi wake mkuu aliweka sauti yake kwenye korasi ya wimbo wake  na DJ Seven 'Say Yes' na kumsifia sana huku aitaja sauti yake kama ya kupendeza.

"Eid Mubarak watu wangu wimbo wa  @djsevenworldwide ft Single Boy  & Esma  #SAYYESS umetoka. Sasa sikutaka kusema hili lakini lazima nimtambue malkia. Hizo sauti za kike za chini zilizo pendezesha hapo kwenye baby kitendawili,, Tega!! Naziona Popo Mbili.. Macho Esma alifanya," aliandika kwenye Instagram.

Bosi huyo wa Konde Music Worldwide alimshukuru Esma kwa kuchangia kwenye wimbo huo na kwa upendo na urafiki wao.

"Asante kwa upendo safi na urafiki Chima. Mungu akubariki," alisema.

Katikati mwa mwezi Februari, video ya Esma akifurahiya wimbo mpya wa Harmonize ‘Single Again’ iilivuma kwenye mitandao ya kijamii.

Kwenye Mahojiano, aliweka wazi kwamba yeye kwa kawaida hucheza nyimbo za wasanii wengi wa Bongo  bila upendeleo, jambo ambalo wanafamilia wake wanafahamu.

"Huwa naimba nyimbo za Alikiba, naimba za Marioo,naimba nyimbo za Harmonize. Sijaona kitu kibaya kwetu na hamna mtu aliyenikasirikia," alisema.

Mapema mwaka huu, dada huyo wa Diamond aliweka wazi kwamba hatajali kuolewa tena, lakini akasema kwamba ana masharti fulani magumu ambayo mwanaume anayemtaka lazima atimize.

Mwaka wa 2020, mama huyo wa watoto wawili aliolewa kama mke wa tatu na Maulid Msizwa.

Ndoa ya Esma ilidumu miezi mitatu tu baada ya sherehe ya harusi yake ya kifahari.

Miezi kadhaa iliyopita, Esma alisema kwamba amezama kabisa kwenye dimbwi la mahaba na anatarajia kuolewa hivi karibuni.

Alimtaja mwanamume wake kama mwanaume mwenye akili zaidi kuwahi kutokea.

"Yeye ni mchapakazi na ana akili kila wakati na sura yake ni ya kufa," alisema, na kuongeza kuwa yuko tayari kutumia maisha yake yote pamoja.

"Ndoa yangu ijayo haitadumu miezi mitatu kama ile ya awali. Siwezi kuchumbiana na mtu ambaye hawezi kuniinua."