Akothee atamani kujaribu mahaba ya Diamond na Fantana na mumewe Denis Shweizer

"Nime'miss mikono yako yenye nguvu na busu zisizohesabika" Akothee alimwambia mkewe.

Muhtasari

•Akothee amekiri kwamba amem'miss sana mumewe Dennis Shweizer baada ya takriban mwezi mmoja bila kuonana.

•Akothee alimfahamisha mumewe kuwa anataka kumdekeza na mapenzi kama jinsi Diamond Platnumz alivyomfanyia Fantana.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji na mjasiriamali Akothee amekiri kwamba amem'miss sana mumewe Dennis Shweizer baada ya takriban mwezi mmoja bila kuonana.

Wawili hao walifunga pingu za maisha katika harusi ya kufana iliyoandaliwa jijini Nairobi mnamo Aprili 10 kabla ya Shweizer ambaye ni maarufu kama Mister Omosh kuelekea Uswizi siku chache baadaye kwa sababu za kikazi.

Katika taarifa yake siku ya Jumatano, mama huyo wa watoto watano alieleza jinsi alivyotazamia kwa furaha kukutana tena na mume huyo wake mzungu baada ya kukamilisha ziara yake kwa wanawe nchini Ufaransa.

"Nimetamani mikono yako yenye nguvu na busu zisizohesabika. Lugha ya mguso ni muunganisho halisi wa kile mwanamke anahitaji. Imekuwa siku 27 na inahisi kama miaka. Nimemaliza kazi na watoto. Sasa sakafu ni ya sisi wawili," Akothee alisema kwenye Instagram na kuambatanisha na picha zake za kumbukumbu na Shweizer.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 alimfahamisha mumewe kwamba anataka kumdekeza na mapenzi kama jinsi Diamond Platnumz alivyomfanyia Fantana kwenye kipindi cha Young, Famous and African.

"Nataka kukudekeza jinsi Diamond alivyomfanyia Fantana. Nimejifunza mtindo mpya wa kubusiana kwenye Netflix nataka kufanya mazoezi nawe," Mwanamuziki huyo alimwambia mumewe.

Katika kipindi cha takriban wiki moja iliyopita, Akothee amekuwa akifurahia muda na wanawe, Prince Ojwang na Prince Oyoo.

Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 aliwatembelea wawili hao ambao wanaishi na baba mtoto wake wa mwisho nchini Ufaransa wiki iliyopita kabla ya kuelekea Switzerland ambako atakutana na mumewe Denis Shweizer.

Siku ya Jumanne, alionyesha video yake na mwanawe Prince Ojwang katika mkahawa ambapo walipata vinywaji.

Takriban wiki mbili zilizopita, mwanamuziki huyo alifichua kuwa mume wake Denis Shweizer almaarufu Omosh alimwagiza aache kazi, aondoke kwenye mitandao ya kijamii na aondoke Kenya ili kuwa naye.

Pia alitangaza mpango wake wa kuchukua mapumziko kutoka kwa mitandao ya kijamii huku akieleza kwamba madhumuni ya mapumziko hayo ya muda usiobainishwa yatakuwa kuangazia kuongeza mtoto mwingine.

Aliwaomba mashabiki wake wamruhusu achukue mapumziko akisema anataka kupata mtoto wake wa sita hivi karibuni.

"Sasa nyie mnipe muda. Nitapumzika kutoka kwa kila mtu na kila kitu pamoja na mitandao ya kijamii. Mniruhusu nitafute mtoto wangu wa pili kutoka mwisho, kabla hatujazungumza mambo mengine.  Nataka kuwa mama mwaka huu," Akothee alisema kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.

Akothee na mchumba wake Dennis Shweizer almaarufu Mister Omosh walifunga pingu za maisha katika harusi ya kifahari iliyofanyika Windsor Golf Hotel & Country Club, jijini Nairobi mnamo Aprili 10.