Malkia wa muziki wa Kenya Nadia Mukami kwa sasa ni mama mwenye hasira kubwa baada ya blogu moja ya humu nchini kuripoti habari za uwongo kuhusu kifo cha mtoto wake mdogo, Haseeb Kai.
Katika taarifa yake ya siku ya Jumapili asubuhi, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 26 alifutilia mbali ripoti kwamba yuko katika hali ya kuomboleza baada ya mwanawe wa miezi 14 kuaga dunia.
Nadia aliashiria hasira yake kutokana na ripoti hiyo na kuwataka mashabiki wake wamsaidie kuripoti blogu iliyoeneza uvumi huo kwa mamlaka husika.
'Naomba mnisaidie kuripoti ukurasa huu wa kijinga!! Mungu amwadhibu mwenye ukurasa huu! Rudi kwa mtumaji!! Tafadhali mnisaidie kuripoti ukurasa huu!!,"Nadia alisema na kuambatanisha na screenshot ya ripoti hiyo ya uwongo.
Mzazi mwenza huyo wa mwimbaji Arrow Bwoy alieleza kwamba alipoamka Jumapili asubuhi alipata jumbe nyingi kwenye simu yake kutoka kwa watu waliojawa na wasiwasi baada ya kukumbana na ripoti hiyo ya uwongo.
"Lazima uwe msaidizi wa shetani kuandika au kufikiria mambo kama haya!!," Nadia alisema akimlenga mwandishi wa ripoti hiyo.
Blogu moja ilichapisha habari za uwongo ikidai kuwa Nadia Mukmi alikuwa akiomboleza baada ya mtoto wake kufariki kutokana na Pneumonia.
"Uchungu wamama huku Nadia Mukami akipoteza mtoto wa miezi 14 kutokana na Pneumonia- Hivipunde TV," kilisoma kichwa cha habari hizo.
Akizungumza kwenye mahojiano na kituo cha runinga cha NTV siku ya Ijumaa, malkia huyo wa muziki aliweka wazi kwamba mwanawe anaendelea vizuri na ameendelea sana katika ukuaji wake.
"Ni mzuri sana. Sasa hivi ni mvulana mkubwa. Anaongea sana na anapenda kucheka sana. Sasa hivi naithamini safari ya uzazi na kusema kuwa na mtoto ni nzuri sana," alimwambia mtangazaji Amina Abdi.
Arrow Bwoy kwa upande wake alifichua kuwa mtoto wao anawaweka bize nyumbani kwani kila mara anadai kushughulikiwa.
Wanandoa hao mashuhuri walibarikiwa na mtoto wao wa kwanza pamoja, Haseeb Kai Machi mwaka jana na wamekuwa wakimlea kwa upendo.