Staa mkongwe wa Bongo Flava, Rehema Chalamila maarufu kwa jina la Ray C yuko tayari kupata mtoto wa pili, baada ya kumkaribisha mtoto wake wa kwanza miezi michache iliyopita.
Mwimbaji huyo mashuhuri mwenye umri wa miaka 41 tayari ameweka ratiba ya lini hilo litafanyika, pamoja na jinsia ambayo anapendelea kwa mzaliwa wake wa pili.
Ray C alifichua hayo kupitia kipande cha video alichoshiriki kwenye hadithi zake za Instagram, alipokuwa kwenye duka fulani la nguo lililokuwa likiuza nguo za watoto wa kike.
Aliiambatanisha zaidi na nukuu inayosema kwamba sasa anataka binti, ambaye anatarajia kuwa naye mwaka ujao.
“KUOMBEA MSICHANA MWAKA UJAO HEHE” Ray C aliandika.
Ray C alimkaribisha mtoto wake wa kwanza ulimwenguni katikati ya Februari 2023.
Msanii huyo kutoka Tanzania alimkaribisha mtoto wa kiume na mpenzi wake, na akamwita Shah Rukh.
Akitangaza habari njema kisha alishiriki picha ya mtoto mchanga, na akaisindikiza na nukuu inayosema:
"Naitwa mama Shahrukh".
Mwanamuziki huyo alifichua ujauzito wake mnamo Februari 7, na kuelezea jinsi alivyojitahidi kuuweka siri.
Kwenye ukurasa wake wa Instagram, Ray C alichapisha video iliyoonyesha tumbo lake likiwa limechomoza sana.
"Wakati wa Mungu ni wakati sahihi," aliandika chini ya video hiyo.
Mwimbaji huyo kwa sasa anaishi na mume wake mzungu nchini Ufaransa. Alihamia nchi hiyo ya Ulaya miaka michache iliyopita na kwa muda mrefu amekuwa akiweka maisha yake ya kibinafsi kuwa siri.
Shahrukh ni mtoto wa kwanza wa Ray C. Takriban miaka minne iliyopita alifunguka kuhusu ujauzito wake kuharibika.