Sonko ampa kazi Conjestina Achieng na familia yake

Hapo awali, Sonko aliahidi kumwajiri Conje kama mkuu wa Usalama katika Klabu ya Volume Inayomilikiwa na Sonko lakini akabadilisha mawazo yake dakika za mwisho.

Muhtasari

• Sonko alisema Conjestina ataendeleza maisha na kukimu familia yake.

• Kulingana na gavana huyo wa zamanani Conje hatarudi Siaya tena atakuwa tu anaenda kusalimia jamaa zake chini ya uangalizi. 

Sonko aajiri Conjestina pamoja na familia yake.
Sonko aajiri Conjestina pamoja na familia yake.
Image: Instagram

Aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko ametimiza ahadi yake ya kumwajiri bondia wa zamani Conjestina Achieng baada ya kuruhusiwa kutoka Rehab.

Mnamo Jumanne, Juni 13, 2023, Sonko alitangaza kuwa ameajiri Conje kama mwongozaji wa mazoezi na mkuu wa usalama katika Salama Bling Beach Resort, Kanamai.

Bosi huyo wa zamani wa Kaunti pia alitaja kuwa Conje atakuwa akifanya kazi katika kituo hicho pamoja na dada yake, mwanawe na kocha.

"Conje atasimamia mazoezi ya kunyanyua vyuma na mkuu wa usalama katika Salama Bling Beach Resort, Kanamai. Pamoja na dada yake, kocha, na mwanawe, tulikagua hoteli atakayofanyia kazi na wote walikubali.

Sasa atakuwa akiendeleza maisha ili kukimu familia yake, lakini tumeelewana nao kwamba Siaya hatarudi tena atakuwa anaenda kusalimia chini ya usimamizi na kurudi," Mike Sonko alisema.

Hapo awali Sonko aliahidi kumwajiri Conje kama mkuu wa Usalama katika Club Volume inayomilikiwa na Sonko lakini akabadilisha mawazo yake dakika za mwisho.

"Mpango wangu wa awali kwa Conje baada ya kupona ulikuwa ni kumwajiri kama Mkuu wa Operesheni za Usalama katika Klabu ya Volume ya Kimataifa lakini nilibadilisha mawazo yangu baada ya kufikiria kuhusu yale ambayo alipitia hapo awali juu ya matumizi ya dawa za kulevya. Sitaki awe karibu na mazingira yoyote yanayohusiana na dawa za kulevya.

Wakati Conje anapoanza sura hii mpya ya maisha yake, anabeba matumaini na ndoto za mabondia wachipukizi. Hadithi yake inatumika kama ukumbusho kwamba kila mtu anastahili nafasi ya kujidhihirisha, bila kujali hali zao za zamani au za sasa,” Sonko alisema.

"Hadithi ya Conje ni moja ya matumaini ya mpiganaji ambayo inakataa kuzimwa. Licha ya kukabiliwa na changamoto na vikwazo maishani, amerejea akiwa na nguvu na dhamira kuliko hapo awali.

Baada ya miezi 11 ya kuokolewa na mike Sonko, hatimaye Conjestina ameonyesha ishara za kupata nafuu na kurejea kwa ndondi.