Mbona wanaume hutaka kujua kuhusu 'body count' ya mrembo kabla ya kumuoa?

Mwanamke aliyeshiriki mapenzi na wanaume Zaidi ya 10, ana asilimia kubwa ya kutalikiwa kwenye ndoa na walioshiriki mapenzi na mwanaume kati ya 0-1 wana asilimia kubwa ya kudumu kwenye ndoa.

Muhtasari

• Katika suala hili, kama unavyoweza kutabiri, wanaume na wanawake walitofautiana pakubwa kwa maoni.

• Wanaume walisema ni sahihi kwa mwanamume kujua penye anawekeza ndoto zake za maisha huku warembo wakisema swali hilo ni kumkosea mtu heshima.

Kuna umuhimu upi kwa mwanaume kutaka kujua idadi ya wanaume mrembo amelala nao?
BODY COUNT Kuna umuhimu upi kwa mwanaume kutaka kujua idadi ya wanaume mrembo amelala nao?
Image: BBC NEWS

Kabla ya kudadavua sababu zinazowafanya wanaume wengi kutilia maanani katika body-count ya wapenzi wao, mwanzo ni vizuri upate uelewa wa ndani kuhusu body-count ni nini.

Kwa ufupi, ‘Body count’ ni idadi ya watu unaofanya nao ngono. Haijalishi jinsi kitendo hicho kilivyokuwa cha karibu, au ni kiasi gani umefanya na mtu, ikiwa hakujawa na kuingiliana, haihesabiki kama ngono katika muktadha huu. Idadi ya miili hapa inarejelea tu idadi ya watu ambao umefanya nao ngono ya kuingiliana.

Swali ni je, kuna umuhimu upi katika wanaume wengi kuweka mkazo katika kutaka kujua idadi ya wanaume ambao mrembo ameshiriki mapenzi nao kabla ya kufanya uamuzi wa kuanza maisha nao kama wake zao?

Swali hili aghalabu hutoka upande wa mwanaume haswa katika uhusiano mpya, utapata tu mwanaume wako anaibuka na swali, “Umelala na wanaume wangapi katika maisha yako?”

Katika Makala haya, tuliweza kuchukua maoni mbai mbali kutoka kwa watu, na kama ilivyo kawaida, wanaume wengi walionekana kutetea swali hilo wakiwa na sababu zao huku kina dada wakidai kwamba swali hilo halina mantiki katika kile walisema kila mtu ana maisha yake ya jana na si vizuri kurudi katika upekuzi wa jana ya mtu.

Mmoja, mwanaume, alisema kwamba kujua idadi ya wanaume ambao mrembo amelala nao ni sahihi ili kukusaidia kama mwanaume kukadiria muda ambao ndoa yako itaweza kudumu – akinukuu utafiti kwamba wanawake waliolala na wanaume wengi wana nafasi finyu sana katika kudumu kwenye ndoa.

Kulingana naye, utafiti ambao hata hivyo hakuutaja ulifanywa na nani, unaonesha kwamba mwanamke aliyeshiriki mapenzi na wanaume Zaidi ya 10, ana asilimia kubwa ya kutalikiwa kwenye ndoa huku wale walioshiriki kitendo na wanaume kati ya 3-9 asilimia yao ya kutalikiwa ni ya wastani.

Wanawake waliowahi kushiriki mapenzi na mwanaume kati ya 0-1 wana asilimia kubwa ya kudumu kwenye ndoa.

Mwingine alisema kuwa wanaume hawapaswi kulinganishwa na wanawake na kudai kwamba kwa macho na mawazo ya mwanaume, anaona mke wake kama uwekezaji wa siku nyingi zijazo na hivyo ni sharti abaini ni wangapi walipita mbele yake.

Lakini kwa upande wa pili kina dada walipinga vikali wakisema kuwa wanaume wanawadunisha kwa kuwataka waeleze idadi ya wanaume waliolala nao, wakati wao hawana haja ya kujua na hata wakijua hawatilii maanani sana suala hilo.

Mmoja alisema kuwa si vizuri mtu kufanya upekuzi kwa maisha ya jana ya mtu kwani kama umeamua kutulia naye kama mke wako, suala la kujua ni wanaume wangapi alishiriki nao kabla yako halina maana yoyote.

“Wanaume ambao mwanamke amelala naye katika siku za nyuma haipaswi kuwafanya ghafla wasivutie kwako, na haipaswi kuathiri msimamo wao na wewe. Wanawake hawafikirii idadi ya wanawake ambao mwanaume amekuwa nao kabla ya kuwapenda inavyopaswa. Kwa nini hawawezi kupewa adabu sawa,” mmoja aliuliza.

“Kweli, ni rahisi; ikiwa unafikiri yeye ni mkarimu, mwerevu, mwenye akili na anayefurahisha kuwa naye, je, body-count yake inabadilishaje ghafla misisimko yote chanya unayohisi ukiwa naye?” mrembo mwingine alihoji.

Maoni yako ni yepi kuhusu body-count ya mtu kabla ya kufanya uamuzi wa kuoana?