Mwimbaji wa nyimbo za injili Peter Omwaka almaarufu Guardian Angel amewashauri wanandoa kufahamiana vyema na kuelewana.
Akizungumza kwenye chaneli yao ya YouTube ya Guardian na Esther, mwanamuziki huyo alidokeza kwamba kuelewa ni nini kila mmoja hufanya vizuri zaidi huwasaidia wanandoa kufurahia ndoa.
Alisema baada ya mtu kujua anachofanya vizuri mwenzie, wapenzi wanapaswa kushikana pamoja na kukamilishana.
“Kwangu mimi kufurahia ndoa ni wewe tu kujifunza wewe ni nani, unajifunza kile ambacho mtu mwingine anaweza kufanya bila tatizo. Unajifunz una uwezo gani, na mwenzako ana ustadi gani halafu mnakuja pamoja kukamilishana,” Guardian Angel alisema.
Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 35 aliwasihi wanaume kuishi maisha yao kulingana na viwango vyao wenyewe na sio kulingana na viwango vilivyowekwa na wanaume wengine.
Aidha, aliwataka kuwufungia masikio wakosoaji na mambo mabaya ambayo watu wanasema kuwahusu wanapoamua kuishi maisha yao halisi wanavyotaka yawe.
“Kama ni mazungumzo ya wanaume kusikiza vile wengine wanasema, wanawake pia waende wasikilize mazungumzo ya wanawake wenzao wakuletee pia. Anaweza akasema vile kwa fulani wako na kitu Fulani, pia wao wanataka ufanye vile wanafanya,” alisema Guardian Angel.
Mwimbaji huyo na mkewe Esther Musila walikuwa wakizungumza kuhusu iwapo wanaume wanapaswa kuchukua majukumu ya kupika wakati mada ya kuishi maisha ya mtu mwenyewe ilipoibuka.
Guardian Angel aliweka wazi kuwa yeye binafsi hana tatizo lolote na kupika na hata akadokeza kuwa anafurahia kufanya hivyo.
"Sina shida na kupika, nitapika. Niko sawa napika, sioni tatizo hapo.. sihisi kama mwanaume kupika inafanya heshima yake irudi chini,” alisema kabla ya kuendelea kupika akisaidiwa na mkewe ambaye alikuwa naye jikoni.
Aliongeza, “Kama utamaduni wetu hauruhusu wanaume kupika, basi wanaume tutokeni kwa kazi ya upishi kabisa. Tuachie wamama wakipika kwa mahoteli sisi tukae kukua tu."
Bi Musila alithibitisha kuwa mumewe Guardian Angel huwa anampikia na akadokeza kuwa ndiyo sababu ya mwili wake kuonekana mzuri.
Guardian na Esther Musila wamekuwa pamoja kwa takriban miaka mitatu sana na walifunga ndoa rasmi mapema mwaka jana.
Wawili hao wamekuwa wakionyesha mapenzi yao kwa kila mmoja licha ya ukosoaji mkubwa kutoka kwa jamii, suala kuu likiwa tofauti kubwa kati ya umri wao ambapo Bi Musila anafahamika kumzidi umri mumewe kwa takriban miaka 20.