Siku ya Jumatatu, mume wa Akothee, Denis Shweizer almaarufu Omosh alilazimika kueleza kwa nini hawakuwahi kufanya harusi ya pili nchini Uswizi kama walivyokuwa wameahidi hapo awali.
Mapema mwaka huu, Akothee na mumewe walikuwa wameahidi kufanya harusi ya pili katika nchi ya nyumbani ya Shweizer, Uswizi ili wanafamilia na marafiki ambao hawakuhudhuria harusi ya kwanza iliyofanyika jijini Nairobi mnamo Aprili 10 kupata nafasi ya kuwaona wakifunga pingu za maisha.
Shabiki mmoja kwenye mtandao wa Instagram alimuuliza mwanaume huyo mzungu kama bado kuna mipango kuhusu harusi ya pili.
"Omosh bado tuna harusi nyingine?," mtumiaji wa Instagram alimuliza Bw. Shweizer.
Huku akimjibu shabiki huyo, Bw Shweizer alidai kwa utani kwamba yeye na mama huyo wa watoto watano walitalikiana mara baada ya harusi yao.
"Tuliachana tarehe 11 Aprili," Shweizer alisema.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya Akothee pia kutoa jibu sawia na la mumewe baada ya kuulizwa swali kama hilo.
Wiki iliyopita, Akothee alionekana kujawa ghadhabu baada ya kuulizwa kuhusu mipango ya harusi yake ya pili na Bw. Shweizer.
Chini ya moja ya machapisho yake, shabiki alimuuliza kuhusu mipango ya harusi hiyo ambayo awali alisema kuwa ingefanyika Julai.
“Madam Boss hatujasahau ile harusi yako kubwa ya majuu, kwani ni lini,” mtumizi wa mtandao wa Instagram alimuuliza Akothee.
Katika jibu lake, mama huyo wa watoto watano alisema kwa kejeili kuwa alitengana na mume wake Denis Shweizer mara tu baada ya harusi yao ya kwanza iliyofanyika jijini Nairobi mnamo Aprili 10 mwaka huu.
Msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 pia alitaka mwanamitandao kuangazia maisha yake mwenyewe na kusonga mbele.
"Tuliachana tarehe 11 Aprili, sasa chukua maisha yako na uendelee," alijibu.
Baada ya harusi yao ya kwanza mwezi Aprili, Akothee alitangaza kuwa wangefanya harusi ya pili nchini Uswizi Julai, mwezi uliopita.
Katika tangazo lake, Akothee alisema angepeleka kikosi chake kizima cha wapambe hadi Uswizi kwa sehemu ya pili ya harusi.
Wakati huo, mama huyo wa watoto watano alifichua majina 17 ya watu ambao wangepamba hafla hiyo ya pili wakiwemo mabinti zake watatu; Vesha Okello, Rue Baby na Fancy Makadia. Wengine ni pamoja na mbunge wa Lang'ata Jalang'o, Kabi na Milly Wajesus, Azziad Nasenya, Mimi, Janet Otieno, Nina Ajigo, Fiona Morema, Lulu, Mokeira Onchiri, Evander Holyfield, Beatrice Schnelli Okello na Geret.