"Alikuwa mwizi!" Mulamwah amshutumu Ringtone kwa kuwauzia wanafunzi CD tupu, t-shirts mbovu

Mulamwah alimshutumu Ringtone kwa kuuza diski tupu na t-shirts zisizo na ubora kwa wanafunzi wasiojua.

Muhtasari

•Ringtone alimshutumu Ringtone kwa kuuza diski bila muziki wowote kwa wanafunzi ambao hawangejua hadi wafunge shule ili kuzijaribu.

“Hakuna injili ambayo ulieneza. Alikuwa na CD moja wakati zingine ameprint picha zake haziibi, na zingine ni za reggae," Mulamwah alilalamika.

Mulamwah na Ringtone walipopatana jijini Nairobi.
Image: YOUTUBE// MULAMWAH

Hivi majuzi, mwanamuziki Ringtone Apoko na mcheshi David Oyando almaarufu Mulamwah walikutana jijini Nairobi ambapo walifurahia wakati mzuri na kushiriki mazungumzo.

Wasanii hao wawili walishiriki vicheko huku wakishambuliana kwa maneno kila na kutaniana kuhusiana na masuala kadhaa kuhusu maisha ya kila mmoja wao.

Ni wakati huo ambapo Mulamwah alimshutumu mwimbaji huyo wa nyimbo za injili kwa kuwalaghai wanafunzi alipokuwa akisoma katika Shule ya Upili ya St Anthony Boys mjini Kitale.

“Huyu msee ametoka mbali. Alikuwa mwizi. Alikuwa anaimba injili lakini alikuwa anatuibia. Alikuwa anakuja shuleni anatuibia,” Mulamwah alilalamika.

Baba  huyo wa binti mmoja alimshutumu Ringtone kwa kuuza diski bila muziki wowote kwa wanafunzi ambao hawangejua hadi wafunge shule ili kuzijaribu.

 “Ulikuja St Anthony Boys nikiwa form 2. Ulikuja na Toyota Seneca, ilikuwa inafungua macho hivi, unatung’aria kabisa. Ulikuja na madisk kwa gunia, eti umekuja kutuuzia. Tukanunua zote. Na zote zilikuwa tupu. Hakuna ilikuwa na ngoma. Alituuzia cover huyu jamaa!” alilalamika.

Aliongeza, “Ulikuwa unajua tuko shule hakuna DVD tutatest nayo ngoma zako. Unatuuzia maempty tunafika nyumbani haiimbi.”

Katika utetezi wake, mwimbaji huyo wa nyimbo za injili alidai kuwa kasi ya juu ambayo muziki uliwekwa kwenye diski hizo ilifanya zisicheze kwa kutumia mashine duni zinazotumika kijijini.

“Ziliburniwa na speed ya juu, mashine za Waluhya za kijijini hapo za China haziwezi kusoma CD imeburniwa na speed ya juu,” alisema Ringtone.

Mulamwah hata hivyo alisisitiza kuwa mwimbaji huyo wa nyimbo za injili alikuwa akiuza diski bila muziki huku akiweka muziki wa reggae katika baadhi yazo.

“Hakuna injili ambayo ulieneza. Alikuwa na CD moja wakati zingine ameprint picha zake haziibi, na zingine ni za reggae. Huyu msee. Zilikuwa na reggae ndani,” alisema.

Ringtone alizidi kujitetea kwa kusema, “Ukweli ni kwamba CD zilikuwa zimeburniwa na speed ya juu, mashine zenu zilikuwa chini. Wale walikuwa na laptop hiyo time, zote zilicheza. Ukweli ni huo.”

Aidha, Mulamwah alimshutumu mwimbaji huyo wa ‘Tenda Wema’ kwa kuwauzia wanafunzi t-shirt zilizotengenezwa kwa nyenzo za mwavuli.

“Material ya mwavuli Ringtone unauzia wanafunzi kweli?” alisema.

Ringtone hata hivyo alijitetea akisema kuwa nguo alizowauzia wanafunzi zilikuwa bora na hazikuwa ghushi kamwe.

Pia alijigamba kuwa aliwatia moyo wanafunzi wa shule ya zamani ya Mulamwah mjini Kitale kushinda mashindano ya soka ya Shule ya Upili na akadokeza kwamba anapanga kurejea huko ili kuhamasisha kizazi kingine cha wanafunzi.