Harmonize kususia ngono siku 30, afichua itakavyomsaidia katika mahusiano yake yajayo

Harmonize alisema uhusiano wake ujao utakuwa wa kudumu na hivyo anataka kuwa makini zaidi kuuhusu.

Muhtasari

•Ijumaa, Konde Boy alifichua kuwa yuko katika siku yake ya sita ya kampeni hiyo ambayo imedhamiria sana kukamilisha.

•Harmonize alisema kukaa siku 30 bila mapenzi itamsaidia kubaini kama anaweza kuvumilia atakapokuwa mbali na mpenzi wake ajaye kwa muda mrefu.

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Staa wa Bongo, Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize yuko kwenye kampeni ya kutofanya mapenzi kwa siku 30.

Katika taarifa fupi siku ya Ijumaa, Konde Boy alifichua kuwa yuko katika siku yake ya sita ya kampeni hiyo ambayo imedhamiria sana kukamilisha.

Bosi huyo wa Konde Music Worldwide alibainisha kuwa kampeni hiyo ni muhimu sana kwani itamsaidia kubaini kama yuko tayari kwa mahusiano yake yajayo ya kudumu.

“Sema hapana kwa Ngono kwa siku 30, Siku ya 6. Hiki ni kipimo tosha cha kujipima na mahusiano yangu ya milele yafwatayo. Yaani nikivuka hiki kipimo nitaamini nimekomaa,” Harmonize alisema kwenye Instastori zake.

Staa huyo wa bongo alisema kukaa siku 30 bila mapenzi itamsaidia kubaini kama anaweza kuvumilia atakapokuwa mbali na mpenzi wake ajaye kwa muda mrefu.

“Nachukua jiko naweka ndani, maskini ya Mungu mtoto wa watu hata akisafiri wiki mbili inakuwa ni mchezo mdogo kwangu hivyo tu,” alisema.

Siku ya Jumatano, mwanamuziki huyo alithibitisha kuwa bila shaka anaweza kustahimili mwezi mzima bila kufanya mapenzi kwani hata hana mpenzi yeyote kwa sasa.

“Ndio, naweza siku 30 bila kukwichi kwichi! sababu sio na yeyote kwa sasa!! Mapenzi ya mbali,” Harmonize alisema siku ya Jumatano.

Mwimbaji huyo alibainisha kuwa hatamruhusu tena mwanamke yeyote kuishi katika nyumba yake hadi ahakikishe kuwa ndiye mwanamke anayetaka kuoa.

“Hutaona msichana yeyote kwa nyumba yangu hadi awe ndio mwanamke wa maisha yangu. Nitakayemuoa. Mwanamke anayeruhusiwa village ukiachilia mbali familia yangu basi awe mfanya biashara au rafiki yangu tena sio rafiki tu, awe rafiki wa karibu sana (Best Friend For Ever) Na iwe sababu maalum,” alisema.

Wakati huo huo, alifichua kwamba aliamuru mfanyakazi wake wa nyumbani kutupa chochote ambacho kimewahi kuachwa nyuma na mtu yeyote aliyemtembelea nyumbani kwake.

“Konde Village ni nyumba safi!! Kuanzia sasa hakuna chama, hakuna kutembea tembea. Aliyewahi kupita pita, hongera. Kama hujawahi kufika, ndio basi tena,” alisema.

Mahusiano ya mwisho ya hadharani ya Harmonize yalikuwa na muigizaji  wa Tanzania Fridah Kajala Masanja ambayo yaliisha katika mazingira yasiyoeleweka mwishoni mwa mwaka jana. Kabla ya kurudiana na Kajala mapema mwaka jana, alijaribu mahusiano na mwanamitindo wa Australia, Brianna Jai ​​lakini hayakudumu.