Seneta wa kuteuliwa Karen Njeri Nyamu kwa mara nyingine amedokeza kwamba ni ombi lake mke wa kwanza Samidoh, Edday Nderitu kurejea kwa familia yao.
Wakati akijibu maoni ya mashabiki katika kipindi cha moja kwa moja, mama huyo wa watoto watatu alifichua kwamba amekuwa akiomba kila mara kwa mara mambo yaende vizuri katika familia yake na ya mke wa kwanza wa mpenziwe.
Alisema ingawa anafurahi kuwa na mwimbaji Mugithi katika maisha yake, hana raha kabisa kuona mambo si mazuri kwa upande wa Edday.
“Bado naomba mambo yaende sawa kwa pande zote mbili kwa sababu hakuna furaha. Hakuna raha, licha na kuwa naskia poa, naskia vizuri watoto wangu na baba na niko na mwanaume ambaye napenda, naskia vizuri. Lakini si vizuri sana kama vile ingekuwa sawa pande zote zikiwa sawa. Lakini sisi sote ni waumini, tunajua hali zetu ziko mikononi mwa Mungu. Mungu hashindwi vita vyake,” Karen Nyamu alisema.
Seneta huyo wa UDA alidokeza kuwa ni kitendo cha Mungu kuwa Samidoh alimchukua kama mpenzi wake huku akibainisha kwamba alikuwa akiomba kila mara watoto wake kuwa na baba yao.
Alifichua kwamba katika sala zake, kila mara alimwomba Mungu ashughulikie hali iliyoikumba familia yake na mambo yaende sawa.
“Mungu hufanya kazi kwa njia zisizoeleweka. Mimi kuna vile nilikuwa naomba naambia Mungu namwambia ‘ulinipa watoto wazuri, baba yao anawapenda. Ana watoto wengine ambao anawapenda sana, ana mwanamke mwingine ambaye anampenda sana...’
Siku zote nilimwomba Mungu ashughulikie hali hiyo. Nilimlilia kutoka moyoni mwangu. Labda yule mwanamke mwingine naye alilia kwa Mungu kutoka moyoni mwake. Nasema ogopa Mungu. Mungu hupanga mambo yake. Tunatumai matokeo bora tu. Tunatumai mambo yatafanikiwa kwa pande zote mbili. Hatujakata tamaa kwa upande huo mwingine. Bado tunaomba mambo yafanyike,” alisema.
Huku akizungumzia watoto wa Samidoh na Edday kujiunga na shule nchini Marekani, wakili huyo alisema kuwa hao ni watoto wao na ni jambo jema.
Mke wa Samidoh wa miaka mingi, Edday Nderitu kwa sasa anaishi Marekani pamoja na watoto wao. Aliondoka nchini mapema mwaka huu na anaonekana tayari kutulia huko vizuri huku watoto wakiwa wameanza shule huko.