Tanzia! Tasnia ya Bongo katika maombolezo kufuatia kifo cha mwimbaji Haitham Kim

Marehemu amemuacha nyuma mtoto wake mmoja mdogo.

Muhtasari

•Marehemu amekuwa akipokea matibabu maalum katika hospitali ya Rufaa ya Temeke jijini Dar es Salaam baada ya kupata matatizo ya kupumua.

Marehemu Haitham Kim
Image: INSTAGRAM

Mwimbaji wa Bongo Fleva Haitham Kim ameaga dunia.

Kim ambaye katika siku za hivi majuzi amekuwa akipokea matibabu maalum baada ya kupata matatizo ya kupumua aliaga dunia katika hospitali ya Rufaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, mwendo wa saa sita mchana siku ya Ijumaa.

Marehemu amemuacha nyuma mtoto wake mmoja.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya wasanii wa Bongo kuanzisha kampeni ya kuchangisha pesa kwa ajili ya matibabu yake ya gharama.

Inaripotiwa kuwa marehemu alikuwa amekumbwa na matatizo ya kupumua ambapo ilianza kama homa ya kawaida lakini baadaye akawa anakosa pumzi hadi kulazwa.

Mashabiki, marafiki, wanafamilia na watu wengine wa karibu wameendelea kumuomboleza mwimbaji na mwandishi huyo wa nyimbo.

Nandy ni miongoni mwa mastaa ambao wamemuomboleza kwa ujumbe wa kihisia.

“Mungu atupe mwisho mwema @haithamkim. Jamani mdogo sana poleni ndugu, jamaa na marafiki kwa ujumla. Hili ni pigo tasnia. Pumzika kwa amani mama,” aliomboleza Nandy.

Zuchu, Kajala Masanja, Hamisa Mobetto, Mr Seed na Wema Sepetu ni miongoni mwa wasanii wengine ambao wamemuomboleza mama huyo wa mtoto mmoja.

Mungu ailaze roho ya Kim pema peponi.