logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Bahati afichua mamilioni ya pesa alizopoteza katika kampeni za uchaguzi wa 2022

Bahati alisema alikuwa kama mgombeaji huru kwani chama cha Jubilee hakikumpa sapoti yoyote.

image
na Radio Jambo

Habari26 September 2023 - 04:02

Muhtasari


•Bahati alibainisha kuwa licha ya kuwania kiti hicho kwa tiketi ya Jubilee, alikuwa kama mgombeaji huru kwani chama hicho hakikuwahi kumpa sapoti yoyote.

•Bahati alisema kuagizwa kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho siku 10 tu kabla ya uchaguzi kulibadilisha mambo mengi.

Mwanamuziki  mashuhuri wa Kenya Kelvin Kioko almaarufu Bahati hatimaye amefunguka kuhusu kiasi kikubwa cha pesa alichotumia wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022.

Katika mahojiano na mchekeshaji Chipukeezy kwenye kipindi cha Chipukeezy Show, mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 30 alibainisha kuwa licha ya kuwania kiti hicho kwa tiketi ya Jubilee, alikuwa kama mgombeaji huru kwani chama hicho kinachoongozwa na aliyekuwa rais Uhuru Kenyatta hakikuwahi kumpa uungwaji mkono wowote.

Bahati alifichua kuwa alitumia takriban shilingi 27milioni kutoka kwa mifuko yake mwenyewe katika kampeni zake.

“Nilikuwa tu niko Jubilee lakini nilikuwa mgombea huru. Kwa sababu sasa, hata na tiketi hii Jubilee siungwi mkono. Nilipelekwa tu IEBC juu tiketi nishapewa hakuna chaguo lingine, hiyo haingerudishwa nyuma. Njia pekee ilikuwa niirudishe na mimi niseme nimeacha kusimama,” Bahati alisema.

Aliongeza, “Lakini ilikuwa kila kitu niko huru. Nilifanya kampeni na pesa zangu mwenyewe hadi mwisho. Nlitumia takriban shilingi milioni 27.”

Bahati aliwania kiti cha Ubunge wa Mathare katika uchaguzi wa Agosti 2022 na aliibuka nambari tatu nyuma ya Anthony Oluoch wa ODM na Billian Ojiwa wa UDA.

Katika mahojiano hayo, mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili alidai kuwa kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga alitaka tu mgombeaji wa ODM kuchukua kiti hicho na hata alimtaka ajiondoe katika kinyang’anyiro akimuahidi kazi serikalini baada ya wao kushinda urais.

Bahati alisema kuagizwa kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho siku 10 tu kabla ya uchaguzi kulibadilisha mambo mengi kwani wafuasi wake wengi walirudi nyumbani wakijua kuwa jina lake tayari limeondolewa kwenye karatasi ya kupigia kura.

“Hata sijui nilitokea aje hiyo kura nilipata, sijui kabisa. Ilikuwa miujiza,” alisema.

Katika uchaguzi wa mwaka jana wa Ubunge wa Mathare, Oluoch wa chama cha ODM alihifadhi kiti hicho kwa kupata kura 28,098 huku Ojiwa wa UDA akiibuka wa pili kwa kura 16,912. Bahati alifanikiwa kupata kura 8,166 kwa tikiti ya chama cha Jubilee.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved