Akothee aendelea kuzua utata kuhusu uhusiano na Nelly Oaks, ajibu kuhusu kum'cheat mumewe

“Hakuna anayem’cheat yeyote, unafunga mlango mmoja, unafungua mwingine.!" Akothee alibainisha.

Muhtasari

•“Nelly, Nelly Oaks.. nakupikia chakula cha jioni nini?? Kifua cha kuku? , kuku mzima, una mlo gani usiku huu?,” Akothee alimuuliza Nelly Oaks.

•Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 pia alisikika akidai kuwa Nelly Oaks huwa mbaya akiwa na njaa.

na meneja wake Nelly Oaks.
Akothee na meneja wake Nelly Oaks.
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki na mjasiriamali mashuhuri wa Kenya Esther Akoth ameendelea kuwachanganya wafuasi wake kuhusu uhusiano wake halisi na meneja wake Nelly Oaks.

Siku ya Ijumaa jioni, mama huyo wa watoto watano alirekodi video ya moja kwa moja kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Facebook kwa takriban nusu saa na kubainisha kuwa alikuwa akimpikia Nelly.

"Nampikia Nelly wangu," Akothee aliandika kwenye sehemu ya maelezo ya video hiyo ya moja kwa moja.

Wakati wa kipindi hicho ambacho kilirekodiwa kutoka jikoni kwa mwimbaji huyo, alionekana akitayarisha milo kadhaa huku akicheza muziki wa Kijaluo.

Ingawa Nelly Oaks hakuwa jikoni pamoja naye, ni wazi kwamba alikuwa karibu tu kwani mwanamuziki huyo alisikika akiongea naye na kumuuliza anataka kula nini.

“Nampikia Nelly... Nelly, Nelly Oaks.. nakupikia chakula cha jioni nini?? Kifua cha kuku? , kuku mzima, una mlo gani usiku huu?,” Akothee alisikika akisema.

Meneja wake alionekana kukubali kula kuku, wali na saladi kwa chakula cha jioni.

“Na ungetaka chakula chako cha jioni kiandaliwe saa ngapi? Saa sita, saa saba?,” Akothee alisikika akimuuliza Nelly Oaks.

Kisha aliendelea na kupika na kucheza densi huku akirekodi matukio yote. Mtoto mdogo pia alionekana akizungukazunguka kwenye video hiyo ya moja kwa moja.

Wakati wa kipindi hicho cha moja kwa moja, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 pia alisikika akidai kuwa Nelly Oaks huwa mbaya akiwa na njaa.

“Samahani, nilikusahau kwa sababu Nelly wangu ana njaa, na akipata njaa anakuwa mtu mbaya sana,” Akothee alisikika mwanamuziki huyo akiwaomba radhi mashabiki wake baada ya muziki aliokuwa akiupiga kukatika.

Kundi la mashabiki waliokuwa wakifuatilia kipindi hicho cha moja kwa moja walielezea shauku yao na kutaka kujua hali halisi ya uhusiano wake na meneja wake.

Baadhi walisisitiza kuwa huenda wawili hao walikuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na kudai kuwa huenda mwimbaji huyo alikuwa akim’cheat mumewe.

Katika majibu yake, Akothee alisema tu “Hakuna anayem’cheat yeyote, unafunga mlango mmoja, unafungua mwingine. Kuweni na jioni njema. Usiku mwema,"