Mchungaji mmoja wa kike amezua mjadala pevu katika mtandao wa X, awali uijulikana kama Twitter baada ya kutoa ushauri unaochukuliwa na wengi kama wa kupotosha kwa watoto wa kike wanotafuta wanaume wa kuwaoa.
Kwa mujibu wa mchungaji huyo, aliwataka warembo kutojinyima sana au kujibeba kwa njia za kiuhafidhina kwani hiyo tu haitakuletea mwanamume wa kukuoa.
Aliwashauri warembo hao kama wana nafasi ya kuvaa mavazi ya kuvutia yenye bei ghali pamoja na kujirembesha kwa vipodoshi basi wafanye hivyo kwani hiyo ndio njia ya haraka ya kuvutia wanaume.
Pia aliwataka kutokosa kwenda katika mitoko ya tafrija za usiku kwani mara nyingi huko ndiko wanaume wa ndoa hupatikana.
Huku akiwahimiza wanawake watoke kwenda kwa party, mhubiri alizungumza dhidi ya kuwa na nywele asili kama mwanamke. Alisisitiza umuhimu wa kuwa na mawigi na nywele bandia za binadamu.
Kwa maneno yake:
“Biblia inasema yule ambaye anataka marafiki mwanzo lazima ajioneshe kwa njia ya kirafiki. Unakunja uso wako kisa hakuna mtu anakutongoza, Ijumaa usiku uko nyumbani, wiki nzima uko nyumbani tu badala ya kutoka huko nje na kutabasamu ili kuvutia wanaume,” alisema.
“Wakati wenzako wanapigiwa simu huku na kule wakisema nakuja, kule ndio wanapata wapenzi. Jioneshe kwa kirafiki ili kupata marafiki. Halafu unapata uko na nywele ya kiasili kwa nini? Nywele za kiasili itasaidia nini? Ni vizuri kuvaa wigi lako, tumia pesa hizo kwa nywele nzuri, tumia vipodozi, onekana wa kuvutia,” aliongeza.
Alisisitiza kwamba nywele za kiasili haziko sokoni kwa sasa kwani wanaume wengi wanataka wanawake waliojiongeza kwa urembo.
“Tumia wigi ukitafuta mpenzi, ukishaolewa unaweza tupa hilo wigi kwa sababu huna jingine la kutafuta huko nje. Lakini kabla ya kuingia kwa ndoa, usijipate ukiwa asilia. Jitunze,” alisema.
Pia aliwaonya wanawake dhidi ya kuwa waombezi sana kwa wanaume wao bali pia kujaribu kuwa na muda mzuri wa kujivinjari kwenye sehemu nzuri za starehe.