Vera Sidika afunguka kwa nini ex wake, Brown Mauzo hakuhudhuria karamu ya binti yao

Alilazimika kuweka mambo bayana kufuatia mashambulizi mengi kwenye mitandao ya kijamii.

Muhtasari

•Katika maelezo yake, Vera alisema kuwa mzazi huyo mwenzake alialikwa kwenye sherehe hiyo lakini hakufika.

•"Je, kosa langu ni nini? Natakiwa kumbeba na crane, nimlazimishe kuhudhuria siku ya kuzaliwa ya binti yake?? Hapana!!" Vera alifoka.

ameeleza kwa nini Mauzo hakuhudhuria karamu ya binti yao.
Vera ameeleza kwa nini Mauzo hakuhudhuria karamu ya binti yao.
Image: INSTAGRAM

Mwanasosholaiti na mfanyibiashara maarufu wa Kenya, Vera Sidika hivi majuzi aliandaa karamu ya kifahari ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa binti yake wa miaka miwili, Asia Brown.

Siku ya Jumanne, mama huyo wa watoto wawili alishiriki picha na video kadhaa za sherehe hiyo ya kifahari na kama kawaida, wanamitandao hawakusita kutoa maoni yao. Kundi la mashabiki walimpongeza Vera kwa karamu hiyo nzuri na kumtakia Asia heri ya siku ya kuzaliwa huku wengine wakimlaumu kwa madai ya kutomualika mzazi mwenzake, Fredrick Mutinda almaarufu Brown Mauzo.

Kufuatia ukosoaji mwingi, mwanasosholaiti huyo wa miaka 34 aliamua kuvunja ukimya wake na kueleza sababu ya mwimbaji huyo kutoonekana kwenye karamu.

"Nimechoshwa na hili: Biashara ya baba mtoto iko wapi kwenye ukurasa wangu. Nyote hamjui lolote kuhusu kinachotokea,” Vera alisema kupitia Instagram.

Katika maelezo yake ya kutokuwepo kwa baba wa watoto wake, alisema kuwa mzazi huyo mwenzake alialikwa kwenye sherehe hiyo lakini hakufika.

"Nilimwalika kwenye siku ya kuzaliwa ya binti yake ili tu iwe ya kukumbukwa kwa siku yake maalum. Nikae huko, wawe na wakati wao. Hakutaka kujitokeza na alisema halikuwa jambo zuri kwake kuwa kwenye sherehe ya siku yake ya kuzaliwa,” Vera alieleza.

Vera aliongeza, "Je, kosa langu ni nini? Natakiwa kumbeba na crane, nimlazimishe kuhudhuria siku ya kuzaliwa ya binti yake?? Hapana!!"

Mama huyo wa watoto wawili aliweka wazi kuwa Brown Mauzo kuharibu mipango ya kufichua uso wa mtoto wao, Ice Brown haikumfanya asimwalike mzazi huyo mwenzake.

Alisema kuwa alichukua hatua ya kumwalika mwimbaji huyo mzaliwa wa Pwani licha ya kuharibu mipango yake kwani anawachukulia watoto wake kama kipaumbele kikuu maishani.

“Mimi sio mama mbinafsi. Lakini huwezi kumlazimisha mtu kufikiri. Siku ya kuzaliwa sio siku ya kawaida, ni siku maalum ya kusherehekea mtoto wako.

Sitawahi kuikosa kwa ajili ya ulimwengu. Nilikimbia kurudi kutoka Amerika, ili tu nisikose kuhudhuria siku ya kuzaliwa ya binti yangu. Lakini si wote wanaona umuhimu huo,” Vera alisema, akionekana kumtupia vijembe mzazi mwenzake.

Alibainisha kuwa alisukumwa kufunguka kuhusu yote hayo kufuatia mashambulizi mengi kwenye mitandao ya kijamii huku wengi wakidai kuwa alikataa kumwalika mpenzi huyo wa zamani.