Bosi wa lebo ya Konde Music Worldwide Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize amewataka mashabiki kumpa sapoti msanii wake wa zamani Anjella Tz licha ya yote yaliyotokea.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Konde Boy aliwataka mashabiki wake kuendelea kumuonyesha upendo mrembo huyo akibainisha kuwa kila mtu ana mapungufu yake.
"Hakikisheni kuwa mnampa sapoti, hakuna aliye kamili," Harmonize alisema siku ya Jumamosi.
Konde Boy aliambatanisha taarifa yake na picha nzuri ya Anjella na zaidi akaweka wazi kuwa anajivunia yeye.
“Endelea kabisa dada yangu. Najivunia wewe,” alisema.
Hatua hii inajiri siku chache tu baada ya sauti inayodaiwa kuwa ya Anjella akizungumza vibaya kuhusu lebo ya Konde Music Worldwide kuibuka.
Katika sauti hiyo iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, mwanadada anayedaiwa kuwa Anjella alisikika akisema kuwa hata Ibraah anataka kuondoka kwenye lebo hiyo ya Harmonize.
“Mwenyewe Ibraah naskia anataka kuondoka pale. Mngempata Ibraah, anaweza akatapika sana. Naskia anataka kuondoka. Sijui anatumia mbinu gani. Ni muda tu mtaskia Ibraah hayuko pale,” sauti hiyo ilisema.
Sauti ya mwanamke ambaye bado hajathibitishwa kuwa Anjella iliendelea kudai kuwa Kondegang imejaa masaibu na maisha ya huko si rahisi hata kidogo.
“Mambo ya pale, maisha magumu. Yaani ukiwa pale hata umaskini huwa hapo. Huna hata nia, unajiuliza hadi lebo vipi imebadilishwa nini? Yaani hupati hata nia. Anataka abaki na wewe hapo akupe elfu ishirini, yaani hajui watu wana familia, hajui. Hajui watu wanaishi aje, hajal,” sauti hiyo ilisema.
Mwanadada huyo pia alidai kuwa watu wengine wanaomzunguka staaa huyo wa bongo pia huondoka wakati mwingine kwenda kufanya kazi zingine ili kupata riziki.
Anjella hata hivyo bado hajajitokeza kukubali ama kukanusha sauti hiyo kuwa yake.
Harmonize alithibitisha kuwa msanii huyo wake wa zamani angeondoka Kondegang mnamo mwezi Novemba mwaka jana na akatoa wito kwa yeyote ambaye alikuwa tayari kuendelea kutoka alikoachia kumsajili.
“Nilikutana na Anjella akiwa amejikatia tamaa akiwa na ndoto kichwani. Sikujiangalia nina kiasi gani, nilijiamini kwa kuwa wapo watu wanaonisapoti bila kuwalipa senti tano basi watasapoti kipaji cha dada Anjella. Nilichoangalia ni ndoto na hasa za mtoto wa kike.
Nimejitahidi kadiri ya uwezo wangu, najua kuna wenye uwezo mkubwa kunizidi, ukizingatia nimeanza juzi. Kama kunaye anayeweza kumwendelezea kipaji chake ni faraja kwangu, asisite kujitokeza," alisema.
Aidha aliwataka watu kupunguza siasa kuhusu sababu ya kuondoka kwa Anjella na kuweka wazi kuwa hakudai hela zozote kutoka kwake.
Angella alithibitisha kuondoka kwake Kondegang mwanzoni mwa mwaka huu huku akiiga familia hiyo yake ya zamani