Avril atoweka mtandaoni baada ya kufichua matatizo katika mahusiano yake na J Blessing

Mwanamuziki Avril amezima akaunti yake ya Instagram yenye wafuasi zaidi ya milioni mbili.

Muhtasari

•Ni dhahiri kuwa akaunti @theavieway ambayo ilikuwa imethibitishwa na Instagram haikuwepo kufikia siku ya Alhamisi asubuhi

•Avril alikuwa amejitokeza kujitetea na kueleza kwa nini alifikia hatua ya kufunguka hadharani kuhusu yale aliyokuwa akipitia faragha.

Image: HISANI

Mwanamuziki na muigizaji mashuhuri wa Kenya Judith Nyambura almaarufu Avril amezima akaunti yake ya Instagram yenye wafuasi zaidi ya milioni mbili.

Ni dhahiri kuwa akaunti @theavieway ambayo ilikuwa imethibitishwa na Instagram haikuwepo kufikia siku ya Alhamisi asubuhi

Hatua hiyo imekuja baada ya mwimbaji huyo mrembo na mzazi mwenzake, mtayarishaji wa muziki J blessing kuvuma kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii Jumanne jioni na Jumatano kutokana na madai ya dhuluma kwenye mahusiano.

Siku ya Jumanne jioni, Avril alizua wasiwasi miongoni mwa mashabiki wake baada ya kushiriki picha za kutisha za uso wake wenye alama za kupigwa na akaonekana kudokeza kuwa J blessing alikuwa amemvamia na kumpiga. Alikuwa ametumia akaunti ya Instagram ambayo amezima kwa sasa kufichua hali yake.

Baadaye, mama huyo wa mvulana mmoja alijitokeza kujitetea na kueleza kwa nini alifikia hatua ya kufunguka hadharani kuhusu yale aliyokuwa akipitia faragha.

"Siku zote nimekuwa mtu wa faragha sana. Siwezi kamwe kuzungumza kuhusu chochote ninachopitia hata kama ninateswa nacho,” Avril alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram Jumatano asubuhi.

Aliendelea, “Moyo wangu ni mzito sana hivi kwamba ilinibidi kuuambia ulimwengu mambo yangu. Ndiyo, niliona kejeli kuhusu mimi kustahili kila kitu ambacho nimepitia enzi za uhai wangu na nina hakika kutakuwa na kejeli zaidi, lakini pia niliona jumbe za upendo na usaidizi."

Mwanamuziki huyo ziadi aliweka wazi kuwa amemsamehe J Blessing kwa lolote lililotokea kati yao na pia kuwataka mashabiki wake wamsamehe mzazi mwenzake huyo.

"Ninakubali kwamba uhusiano wetu wa miaka saba na safari yetu kama wazazi kwa mvulana mdogo mzuri imekabiliwa na changamoto, na kumekuwa na migogoro ambayo iliongezeka hadi mapigano. Tunatambua hitaji la mabadiliko na tumejitolea kutafuta usaidizi na kujifunza njia bora za kuwasiliana na kutatua masuala. Lengo letu la pande zote mbili ni kujenga mazingira chanya na kusaidiana zaidi, kukuza uelewano na ukuaji,” alisema.

Pia aliweka wazi kuwa hakuwa akitafuta kiki kuhusu suala hilo, kama baadhi ya wanamitandao wa Kenya walivyodai.

Katika utetezi wake, J Blessing alidai kuwa moja ya picha alizochapisha mzazi mwenzake huyo ni tukio lililotokea mwaka jana.

Hata hivyo, alikiri kuwa hapo awali walikuwa na ugomvi uliopelekea vita, na kusababisha majeraha kwa wote wawili ambayo yalitibiwa hospitalini.

“Naomba radhi sana kwa madhara niliyomsababishia Avril au mtu mwingine yeyote. Nina hatia, lakini ningependa kufafanua mambo machache. Karibu mwaka mmoja uliopita, tulikuwa na ugomvi wa kimwili ambapo sote tulijeruhiwa, na siku hiyo, mara moja nilimpeleka hospitali. Ninachukua jukumu kamili kwa wakati huo wa udhaifu. Moja ya picha alizoweka ni za tukio hilo,” J bless alisema.

Aliongeza, “Jana usiku kulitokea hali iliyosababisha ugomvi, lakini haikuwa kipigo kama ilivyopendekezwa. Ninataka kumhakikishia kila mtu kwamba sikumpiga. Mimi si mnyanyasaji, na sikumpiga. Mimi ni binadamu ambaye nilifanya makosa katika maisha yangu."

Mtayarishaji huyo pia alitangaza kuwa yeye na Avril wamekubali kuishi tofauti baada ya tukio la hivi majuzi lililowahusu.