"Najivunia wewe mfalme wangu" Karen Nyamu amsherehekea Samidoh kufuatia mafanikio makubwa

Seneta Karen Nyamu alimtambua mpenzi wake Samidoh kama ‘mfalme’ wake huku akimpongeza.

Muhtasari

•Karen Nyamu alimsherehekea mzazi mwenzake Samuel Muchoki almaarufu Samidoh baada ya kutoa tangazo kubwa.

•Seneta Nyamu alisema alikutana mara ya kwanza na Samidoh katika hafla ya kisiasa ambayo ilifanyika miaka kadhaa iliyopita.

Samidoh na Karen Nyamu
Image: FACEBOOK// KAREN NYAMU

Siku ya Alhamisi, seneta wa kuteuliwa Karen Njeri Nyamu alimsherehekea mzazi mwenzake Samuel Muchoki almaarufu Samidoh baada ya kutoa tangazo kubwa.

Samidoh alishiriki chapisho la shukrani kwa mashabiki wake kwenye Facebook baada ya kufanikiwa kupata wafuasi zaidi ya milioni mbili kwenye mtandao huo wa kijamii.

Katika chapisho hilo, staa huyo wa Mugithi aliwashukuru mashabiki wake kwa sapoti na kuwaomba waendelee na safari pamoja naye.

"Ninahisi kushukuru sana kwa sapoti yenu! Tumefikia wafuasi milioni 2 kwenye Facebook, na yote ni shukrani kwa kila mmoja wenu. Sapoti yako katika kile ninachofanya inamaanisha ulimwengu kwangu. Asante Mungu kwa safari hii. Hapa ni kwa kukua pamoja!,” Samidoh aliandika kwenye bango la shukrani ambalo alichapisha.

Mamia ya watumiaji wa mtandao wa Facebook wakiwemo wasanii wenzake na watu wengine mashuhuri walikusanyika chini ya chapisho hilo kumpongeza na kuahidi sapoti zaidi.

Karen Nyamu ambaye ana watoto wawili na mwimbaji huyo ni miongoni mwa waliotoa maoni ya kumpongeza kwa mafanikio yake. Katika maoni yake, seneta huyo wa kuteuliwa wa UDA alimtaja kama mfalme wake.

"Hongera, ninajivunia wewe mfalme wangu," Karen Nyamu aliandika.

Samidoh na mwanasiasa huyo ambaye maisha yake yamezungukwa na drama tele wamekuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa miaka kadhaa sasa na wawili hao wana watoto wawili pamoja. Wawili hao wameonekana pamoja sana katika miezi michache iliyopita hasa baada ya mke wa kwanza wa mwimbaji huyo, Edday Nderitu kuhamia Marekani na watoto wao watatu mapema mwaka huu.

Siku kadhaa zilizopita, seneta Nyamu alifichua kuwa alikutana kwa mara ya kwanza na Samidoh katika hafla ya kisiasa iliyofanyika miaka kadhaa iliyopita.

Akizungumza kwenye YouTube Channel ya Convo, Karen alifichua kwamba mwimbaji huyo maarufu wa Mugithi alikuwa akitumbuiza katika hafla ambayo alikuwa amehudhuria wakati alipomtambua.

Seneta huyo alisema licha ya kumtambua mwanamuziki huyo, hata hivyo hawakupata fursa ya kuzungumza na kubadilishana namba mara ya kwanza walipokutana.

“Nilikuwa nimeona jina lake kwa YouTube lakini sikuwa shabiki hivyo ati namjua. Tulipatana tu kwa hafla fulani ya kisiasa ambapo alikuwa akitumbuiza, nikamtambua lakini hakuna chochote kilifanyika. Hatukubadilishana hata namba,” Karen Nyamu alisimulia.

Aliongeza, "Pia tulipata fursa nyingine, tukio lingine la kisiasa. Hiyo siku ndio niliona alaa, na kuna vile. Sijawahi kusahau hiyo shoe game kwanza. Ilikuwa juu. Mengine ni historia.”

Seneta huyo wa kuteuliwa wa chama cha UDA alisema wakati alipokutana na mpenzi wake huyo, alicheza naye mchezo wa kujificha na kutafuta kwa mara ya kwanza huku akimpuuza na wakati huo huo kumpa vidokezo.