Mzazi mwenza wa Karen Nyamu, DJ Saint Kevin amefunguka kuhusu mkutano wao wa kwanza kabisa.
Katika mahojiano ya hivi majuzi na kituo kimoja cha redio cha humu nchini, Kevin ambaye ni mcheza santuri na mburudishaji alifichua kuwa walikutana kwenye shoo ambapo alikuwa akitumbuiza.
"Tulikutana katika safu yangu ya kazi, katika Tamasha. Hapo ndipo tulipokutana,” DJ Saint Kevin alisema.
DJ Saint ndiye baba wa mtoto wa kwanza wa Karen Nyamu. Wawili hao walichumbiana kwa kipindi kabla ya kwenda njia tofauti.
Katika mahojiano hayo, mshereheshaji huyo pia alizungumzia uhusiano wake wa sasa na Bi Nyamu ambapo alifichua kuwa wanashirikiana vyema katika uzazi.
“Yeye ni mtu mzuri; yeye ni mama mzuri kwa mtoto wetu. Sisi tunashirikiana katika malezi. Hakuna uhusiano mbaya, sisi ni wazazi wenza,” alisema.
Aliongeza, “Tunaishi maisha tofauti kabisa, yeye ana maisha yake na mimi nina yangu, na niko poa nayo. Tunakutana katikati linapokuja suala la watoto, hiyo ni kama wakati pekee tunakutana."
Aidha, DJ Saint Kevin alikanusha kupata upendeleo wowote wa kimapenzi kutoka kwa seneta huyo wa kuteuliwa akisema, "Hakuna marupurupu, mimi huenda kumchukua mtoto kila wiki na tuko poa. Kisha ninamrudisha, na ndivyo hivyo."
Saint Kevin pia alifichua kuwa amewahi kukutana na mpenzi wa sasa wa Karen Nyamu, Samuel Muchoki almaarufu Samidoh na hata akamminia sifa tele mwimbaji huyo wa Mugithi.
"Nimekutana na yule jamaa, ni mtu mzuri sana. Hakuna uhusiano mbaya," DJ Saint Kevin alisema.
Huku akizungumzia hisia zake kuhusu Karen Nyamu kuwa katika uhusiano mpya, deejay huyo alisema, "Jamaa huyo (Samidoh) alikuja baadaye sana, kila mtu anaruhusiwa kuendelea."
Wakati akizungumza katika mahojiano na Alibaba kwenye Radio Jambo mwaka wa 2021, baba huyo wa watoto wawili alisema alikutana na Karen Nyamu kwenye hafla ambayo alikuwa akitumbuiza kama mcheza santuri.
”Nilikutana na Karen kabla ya kuwa mwanasiasa. Alikuwa wakili na nilikuwa kwenye hafla ya DJ,” alisema.
Miaka mingi baada ya kutengana, Karen baadaye alikutana na mwimbaji Samidoh na wakabarikiwa na watoto wawili pamoja.