Milly Chebby, Terence Creative hatimaye wafunguka kuhusu mzozo na Jackie Matubia

Milly amebainisha wazi kuwa kuna tatizo kwenye uhusiano wake na rafiki yake wa muda mrefu, Jackie Matubia.

Muhtasari

•Milly alibainisha kuwa kutoelewana na muigizaji huyo ambaye amekuwa rafiki yake kwa miaka mingi ni sehemu ya maisha.

•Milly alimualika Matubia kwenye hafla yao ya Washwash 4 Icon ambayo itafanyika Desemba 11 na kusema anatumai atakuwa huko.

Terence Creative, Milly Chebby, Jackie Matubia
Image: INSTGRAM//

Mke wa mchekeshaji Terence Creative, Milly Chebby amebainisha wazi kuwa kuna tatizo kwenye uhusiano wake na rafiki yake wa muda mrefu Jackie Matubia.

Katika mahojiano na Commentator, mama huyo wa mtoto mmoja alibainisha kuwa kutoelewana na muigizaji huyo ambaye amekuwa rafiki yake wa karibu kwa miaka mingi ni sehemu ya maisha.

“Tulikuwa mabeshte sana, tulikuwa tunaitana ‘sisi’ najua kuna watu hapo wamevunjwa moyo, msijali. Siku zote kuna jambo maishani ambalo hutokea ili uweze kufahamu vyema,” Milly Chebby alisema.

Aliongeza, “Wakati mwingine hata unapigana na mumeo na una’miss nyakati ambazo ulikuwa ukishiriki hadithi naye. Unaskia tu uko na mushene inakuwasha alafu unakumbuka alikukosea jana, unang’angana tu na hio mushene yako unakaa nayo. Ni maisha,"

Milly hata hivyo alikanusha madai ya awali kwamba aliwahi kudai kuwa rafiki yake huyo wa zamani hana mume.

“Tulipokuwa marafiki, tulikuwa marafiki sisi wawili tu. Tulipokuwa familia, tulikuwa familia kama tulivyokuwa na iliposimama, kwa kweli sikufikiri kuwa mmoja wetu angeenda hadharani na kusema hiki na kile. Lakini kitu moja kwa kweli, sijawahi kusimama nikasema Jackie hana bwana. Sijawahi,” alisema.

Aidha, mtayarishaji maudhui huyo aliomba ushahidi wowote wa yeye akidai kuwa Jackie Matubia hana mume uwekwe hadharani ikiwa madai hayo ni ya kweli.

Akizungumzia urafiki uliovunjika kati ya mkewe na Bi Matubia, Terence pia alibainisha kuwa migogoro kati ya watu wa karibu ni sehemu ya maisha.

“Kama mtu ni dadako ata mkikosana, bado ni dadako. Pengine tofauti yenu inaweza kuwafanya mkuwe kidogo kidogo kwa muda mkijaribu jee ni ujinga gani hiyo ilitukosanisha na tunasuluhisha vipi? Ni jambo nzuri sana wakati mwingine kukaa kando ndio muweze kuelewana, muweze kuthaminiana ndio muweze kuelewa ni wapi mnakwaruzana kama madada,” Terence alisema.

Mchekeshaji huyo mashuhuri aliwaomba Wakenya waache kusukuma ajenda zenye nia mbaya ambazo si za kweli kwani kutoelewana kati ya marafiki na wapenzi ni jambo la kawaida.

Milly Chebby aliendelea zaidi kumualika Matubia kwenye hafla yao ya Washwash 4 Icon ambayo itafanyika jijini Nairobi mnamo Desemba 11 na kusema kwamba anatumai rafiki yake wa zamani atakuwa huko.