Mume wa Zari, Shakib Lutaaya amsherehekea mwanawe wa kambo kwa njia ya kipekee

Shakib alimsherehekea mwanawe wa kambo Riaz Nasibu Abdul almaarufu Prince Nillan katika siku yake maalum.

Muhtasari

•Shakib alitumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kumsherehekea Prince Nillan alipokuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa.

•Katika video hiyo, wanaume hao wawili walionekana wakitembea pamoja huku tabasamu zuri likionekana kwenye nyuso zao.

Shakib Lutaaya na mwanawe wa kambo, Prince Nillan.
Image: INSTAGRAM// ZARI HASSAN

Mfanyibiashara wa Uganda Shakib Cham Lutaaya mnamo Jumatano alimsherehekea mtoto wake wa kambo Riaz Nasibu Abdul almaarufu Prince Nillan katika siku yake maalum.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 32 ambaye ni mume wa Zari Hassan alitumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kumsherehekea mtoto wa mwisho wa mwanaosholaiti huyo alipokuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa. Prince Nillan alifikisha umri wa miaka saba Jumatano, Desemba 7.

Shakib alichapisha video nzuri iliyoonyesha akitembea bega kwa bega na Prince Nillan huku wakiwa wamevalia suti za kijivu zinazolingana.

"🎂🎁🙏🏻" aliandika kwenye video hiyo.

Katika video hiyo, wanaume hao wawili walionekana wakitembea pamoja huku tabasamu zuri likionekana kwenye nyuso zao.

Shakib ambaye pia aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa mapema wiki hii, Jumanne anaonekana kuwa na uhusiano mzuri na watoto wa Zari Hassan. Mwanasoshoaliti huyo ambaye anaishi Afrika Kusini ana watoto watano ambao alizaa na wapenzi wawili wa zamani, Ivan Ssemwanga na Diamond Platnumz.

Mfanyibiashara huyo na mama huyo wa watoto watano walifunga ndoa rasmi mwezi Oktoba baada ya kuchumbiana kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Jumatano jioni, Zari Hassan aliwasherehekea Shakib na Nillan wakiadhimisha siku yao maalum, siku yao ya kuzaliwa.

Katika ujumbe wake kwa wawili hao, mwanasosholaiti huyo mwenye umri wa miaka 43 alimuomba Mungu atimize matamanio yao yote ya moyo.

"Nisaidieni kuwatakia mume wangu na mwanangu siku njema ya kuzaliwa.. Mwenyezi afanye mapenzi yako yote yatimie," Zari Hassan aliandika kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Aliambatanisha ujumbe wake na picha ya Shakib na Prince Nillan wakiwa wamesimama kando huku wakiwa wamevalia suti za kijivu zinazolingana. Wawili hao walionekana vizuri pamoja.

Shakib alifikisha umri wa miaka 32 Jumanne, Desemba 5 wakati Prince Nillan anasherehekea siku yake ya saba ya kuzaliwa leo hii, Desemba 6.

Prince Nillan ni mtoto wa Zari Hassan na aliyekuwa mpenzi wake, mwimbaji Diamond Platnumz. Kwa upande mwingine, mwanasosholaiti huyo alifunga ndoa rasmi na Shakib katika harusi ya kupendeza mapema mwaka huu. Pengo la umri kati ya mama huyo wa watoto watano na mumewe hata hivyo limekuwa suala kubwa miongoni mwa mashabiki wao tangu uhusiano wao ulipojulikana hadharani mapema mwaka jana.